Bulembo ataka Magufuli apite bila kupingwa

Muktasari:

Mbunge wa Kuteuliwa (CCM) Abdalah Bulembo ametaka kusifanyike uchaguzi wa urais nchini Tanzania na badala yake Rais John Magufuli apite bila kupingwa ili fedha zitakazookolewa ziende katika kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Dodoma. Mbunge wa Kuteuliwa (CCM) Abdalah Bulembo ameutaka upinzani kukubali Rais wa Tanzania John Magufuli apite bila kupingwa ili fedha zilizokuwa zitumike katika uchaguzi ziende kwenye kukabiliana na ugonjwa wa corona.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Bulembo amesema badala ya kumchagua Rais, wapiga kura wawachague wabunge na madiwani tu.
“Sote tunalia corona hapa mara mkakati wa corona. Niwaombe wenzangu wa upinzani waache Magufuli apite bila kupingwa tusiwe na uchaguzi wa urais pamoja na Katiba inasema,”amesema.
Amesema anao uhakika upinzani hawana mgombea urais na kuhoji sasa kwanini watumie gharama kubwa kufanya uchaguzi wakati mshindi wanaye.
“Utekelezaji unaonekana, aliyoyafanya yako wazi. Kipindi kile tulitoka jasho kidogo kwasababu alitoka (Edward Lowasa) na kwenda upande wa pili. Lakini sasa nani yuko huku,  sioni. Kwa hiyo tuvumilie tuchukue fedha zikasaidie corona badala ya uchaguzi wa urais tufanye uchaguzi wa wabunge na madiwani tu,”amesema.
Amesema kikubwa vyama vya upinzani vikipata wabunge wengi au wachache wataongeza kipato.
“Pato linatokana na wabunge halitokani na urais. Mheshimiwa Spika (Job Ndugai) hawa ni rafiki zangu lakini katika hili tukubaliane tu kwamba katika vyama vyote vya upinzani nani atamshinda Magufuli? Amehoji.
Amehoji kwanini wanapoteza fedha wakati wanaenda kushindana na jiwe kwasababu hakuna sababu.
“Tuje huku tuweke utaratibu Magufuli apitishwe tufanye uchaguzi wa wabunge na madiwani. Uchaguzi ni gharama kubwa. Serikali inaumia unapofanya uchaguzi wa Rais gharama yake inatisha. Mimi nayasema kwa dhati. Ninajua wenzangu wapinzani watachukia lakini siku ya mwisho atakuwa ameshinda Magufuli kwa aslimia 85 hadi 90,”amesema.
Amehoji kwanini wapoteze muda na kwamba anaamini kuwa wanaweza kupeleka hoja bungeni ya kumuacha Rais Magufuli aendelee na urais na kufanya uchaguzi wa wabunge na madiwani tu.