Bunge lamkataa Profesa Assad, lamkubali CAG

Dodoma/Dar. Wakati sakata la Bunge kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad likitikisa kila kona, Spika Job Ndugai ameweka msimamo wa chombo hicho. Amesema, “hakuna wakati wowote ambao Bunge limekataa kufanya kazi na taasisi ambayo ni ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad basi.”

Jana, bungeni jijini Dodoma Ndugai aliweka msimamo huo ikiwa ni siku ya tatu tangu Bunge kupitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad, huku pia ikishuhudiwa chombo hicho kikiazimia mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kusimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge.

Uamuzi wa Bunge kuhusu Lema ulisababisha wabunge wa upinzani wakiongozwa na mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutoka katika ukumbi wa Bunge na Ndugai kuagiza wasirejee tena siku hiyo huku akiamuru wanahabari kutowafuata na kuwahoji nje ya viwanja vya Bunge.

Kuhusu kufanya kazi na CAG, Ndugai alianza kwa kusema kuwa anataka kuweka sawa jambo hilo kutokana na hali ya sintofahamu iliyopo na kubainisha kuwa Bunge halifanyi kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad na si taasisi ya CAG. “Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad basi. Tusiripoti tofauti tukauchonganisha umma na kuuchanganya.”

Aprili 2, Bunge lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad kutokana na kauli aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa Bunge ni dhaifu. Kabla ya uamuzi huo, Profesa Assad alihojiwa na kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ilipendekeza Bunge lisifanye naye kazi na hoja hiyo kupita.

Pia, kamati hiyo iliazimia mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge kutokana na kuunga mkono kauli ya Profesa Assad.

Kuhusu Lema, aliadhibiwa baada ya Jumanne iliyopita kupinga adhabu ya Mdee bungeni na kurudia kauli kuwa “Bunge ni dhaifu.” Alipelekwa katika kamati hiyo ya Bunge na juzi alihojiwa na jana kamati ikasoma mapendekezo yake na Bunge kuridhia asimamishwe kuhudhuria mikutano mitatu.

Taasisi ya Wajibu yatoa angalizo

Kutokana na sintofahamu hiyo, Taasisi ya Wajibu inayoongozwa na CAG mstaafu, Ludovic Utouh imetoa taarifa ikisema haionyeshi dalili nzuri za mwendelezo wa uimarishaji wa uwazi na uwajibikaji nchini.

Taarifa hiyo iliyotolewa na bodi ya wakurugenzi imeeleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 143 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (iliyorekebishwa mara kwa mara) pamoja na Kifungu cha 34 (2) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, zinaeleza kuwa, Rais atawaagiza wahusika wawasilishe ripoti za CAG kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge utakaofanyika baada ya Rais kupokea ripoti hizo kabla ya kupita siku saba tangu siku ulipoanza mkutano huo.

“Wajibu inaamini kuwa mbali na sintofahamu hiyo, ripoti za CAG za mwaka 2017/18 zitawafikia wananchi kwa wakati kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo, ili ripoti hizo ziweze kutumika na wadau wa uwajibikaji nchini,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mtazamo wa wanasheria

Akizungumzia sakata hilo, mwanasheria kutoka Crax Law Partner, Hamza Jabir alisema siyo rahisi kumtenganisha Assad na ofisi ya CAG kwa sababu yeye ndiye mtendaji mkuu aliyeteuliwa na Rais kwa mujibu wa katiba.

Alisema kauli ya Spika inachanganya kwa sababu tangu hapo awali hajawahi kufanya kazi na Assad, anafanya kazi na ofisi ya CAG ambayo kwa namna yoyote ile inaendeshwa na Assad kisheria.

“Hili suala ni la kisheria zaidi, anachokisema Spika kikatiba hakipo. Sheria inayoweza kumuondoa Assad (CAG) kwenye kiti ni Katiba, Ibara ya 144 na anayemuondoa ni Rais aliyemteua kwa kuitisha tume maalumu ichunguze na sababu zimeanishwa kwenye Katiba tofauti na hizo hata Rais hawezi kumuondoa.

Mwanasheria maarufu nchini, Harold Sungusia alisema kazi ya CAG ni kuchunguza mapato na matumizi ya Serikali ambayo kazi ya kusimamia hilo inafanywa na Bunge.

Alisema iwapo wataamua kutofanya kazi naye kabisa wanaweza ila haitakuwa na tija iwapo CAG hatawaambia amekagua nini na amekutana na nini.


Habari imeandikwa na Fidelis Butahe (Dodoma), Asna Kaniki, Kalunde Jamal na George Njogopa (Dar)