Kamati ya Bunge yaridhishwa utendaji utendaji kazi wa Shirika la Stamico

Thursday October 31 2019

Waziri wa Madini wa Serikali ya Tanzania, Doto

Waziri wa Madini wa Serikali ya Tanzania, Doto Biteko 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Madini wa Serikali ya Tanzania, Doto Biteko ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa mwenendo wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ni mzuri kwa sasa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Biteko amesema Stamico lina uwezo  wa kutoa gawio kwa Serikali la Sh1 bilioni, hivyo  ameiomba kamati hiyo kuendelea kuiunga mkono wizara yake katika mipango ya kulisimamia na kulifanya kuwa na tija kama inavyotarajiwa.

Waziri huyo ameyasema hayo leo Oktoba 31, 2019 Jijini Dodoma mbele ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati wa kuwasilisha taarifa mbalimbali za Wizara na taasisi zake.

Amesema matatizo makubwa yanayoifanya Stamico kushindwa kwenda kwa kasi kama inavyo tarajiwa, yamewasilishwa kwenye kamati hiyo na mamlaka nyingine ili kupatiwa ufumbuzi.

Waziri Biteko amesema kwa sasa usimamizi wa miradi ya shirika hilo inaonyesha kuwa na tija huku akitolea mfano mgodi wa TAMIGOLD unaomilikiwa na Stamico kwa niaba ya Serikali, ambao unatengeneza faida tofauti na zamani.

Amesema pia gharama za uendeshaji wa mgodi huo zimepungua kutoka Dola 1,800 kwa wakia moja hadi Dola 940 kwa wakia moja.

Advertisement

Amesema mgodi umeweza kulipa madeni mbalimbali kutoka Sh66 bilioni 66 hadi kufikia Sh33 bilioni 33 yakiwamo malipo ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi na wazabuni.

Waziri huyo ameiambia kamati kuwa bado wanaendelea kuongeza mianya ya faida baada ya kuondokana na matumizi ya mafuta watakapo anza kutumia umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Pamoja na hayo, Waziri Biteko amesema kwa sasa mgodi unatumia Sh1 bilioni kwa mwezi kwa ajili ya mafuta wakati hesabu zinaonyesha watakapotumia umeme wa Tanesco, watatumia kiasi cha Sh300 milioni kwa mwezi na wataokoa kiasi cha Sh700 milioni  kwa mwezi.

Eneo lingine alilozungumzia waziri huyo wa madini nchini ni la kuongeza faida kutokana na kuuza madini hapa nchini baada ya kumaliza mkataba wao wa kuuza madini nje.

Amesema mwezi ujao mkataba huo utahitimishwa na gharama zote zinazotumika kwa ajili kusafirisha na gharama nyingi zitakuwa sehemu ya faida.

Akizungumzia kuhusu mradi wa makaa ya mawe pamoja na changamoto mbalimbali, Waziri Biteko amesema bado unaonyesha mafanikio makubwa ukilinganisha na huko nyuma.

Miongoni mwa mafanikio aliyataja ni pamoja na usimikaji wa Mzani ya kupimia makaa ya mawe ambao awali haukuwapo, hali iliyokuwa ikisababisha tatizo.

“Shirika limezalisha jumla ya tani 35,978.40 za makaa ya mawe, liliuza jumla ya tani 16,950.17 zenye thamani ya Shilingi 980,900,000. Mauzo hayo yaliwezesha malipo ya mrabaha wa Shilingi 29,426,440.67, ada ya ukaguzi Shilingi 9,808,813.56 na Ushuru wa Huduma wa Shilingi 2,942,644.07,” amesema Biteko.

Aidha, akizungumzia mradi wa Tanzanite wa ubia kati ya Stamico na Tanzanite One, Biteko amesema wizara yake imesimamia mambo mengi kuhusu mradi huo huku Stamico ikiwa ndiyo msimamizi wa serikali.

Ameiambia Mamati ya Bunge kuwa kipindi cha nyuma walikuwa wanakusanya kilogramu 166 za Tanzanite kwa mwaka, lakini kwa sasa wanakusanya zaidi ya kilogramu 1,670 kwa mwaka.

Kwa upande mwingine, Biteko ameiambia kamati kuwa miongoni mwa changamoto nyingine iliyokuwa inaikabili Stamico ni pamoja na uongozi (management) na muundo wake ambao tayari utatuzi wake umefanyika kwa kuunda muundo mpya ambao utakuwa na kurugenzi tatu badala ya tano na baadhi ya vyeo vimepunguzwa ili kuongeza tija.

Waziri alitolea ufafanuzi wa kubadilisha uongozi wa shirika hilo kuwa hufanyika ili kutafuta ufanisi.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariamu Mzuzuli ameipongeza wizara kwa kazi nzuri, hata hivyo ameishauri kuendelea kuisimamia sekta ya madini pamoja na kutatua changamoto zilipo pamoja na hoja mbalimbali zilizotolewa na wajumbe ili wizara ikazifanyie kazi.

 

 

Advertisement