CAG Kichere atambulishwa bungeni, Spika Ndugai atoa neno

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akitambulishwa bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Novemba 3, 2019, Rais wa Tanzania, John  Magufuli alimteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchukua nafasi ya Profesa Mussa Assad.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemkaribisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere akiahidi Bunge kumpa ushirikiano mkubwa.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 11,2019 akimkaribisha bungeni Kichere ambaye amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Mussa Assad.

Kichere amesimama kwa dakika tatu akitambulishwa na Spika ambapo amehakikishiwa ushirikiano kwa kila kamati.

"Nataka nimuhakikishie kuwa, Bunge litakupa ushirikiano wa kila aina na wala hatuna tatizo na ofisi ya CAG kwa hiyo tutakuwa pamoja," amesema Ndugai.

Spika amesema leo mchana atakutana na CAG na wenyeviti wa kamati pamoja ili wajadiliane pamoja na kuzungumza baadhi ya mambo.

Baada ya kumtambulisha, wabunge wa upande wa chama tawala walipiga makofi kwa uchache lakini hakuna makofi yaliyosikika kutoka upande wa wabunge wa upinzani.

CAG alikuwa ameongoza na watumishi wengine katika ofisi yake ambao Spika aliwatambulisha huku akiwaomba kuisaidia Tanzania kusonga mbele.

CAG aliyemaliza muda wake Profesa Musa Assad aliingia katika mzozo na Bunge na kuitwa mbele ya Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kile kilichoelezwa kutoa kauli ya kudhalilisha muhimili huo kuwa ni ‘dhaifu.’

Taarifa ya kamati ilipowasilishwa bungeni Aprili 2019, Bunge lilipotisha azimio la kutokufanya kazi na Profesa Assad.