CCM wapuliza kipenga uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimetangaza ratiba na utaratibu utakaotumika kuwapata wagombea wake wa uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimetangaza ratiba na utaratibu utakaotumika kuwapata wagombea wake wa uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole leo Ijumaa Oktoba 11, 2019.

Amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kugombea nafasi za uenyekiti wa mitaa, vijiji na ujumbe wa serikali a vijiji na mitaa lilianza Oktoba 7, 2019 na litamalizika Oktoba 12.

Amesema fomu hizo zitachukuliwa kwa makatibu wa matawi ya CCM kote nchini.

Amesema Oktoba 13, 2019  kamati za siasa za matawi zitawajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za kata.

Amesema Oktoba 14 kamati za siasa za kata zitajadili na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za wilaya.

Polepole amesema Oktoba 16 hadi 18, 2019 kamati za siasa za wilaya zitajadili wagombea na kufanya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni na mkutano mkuu wa wanachama wote wa tawi.

Amesema mikutano ya kura za maoni ya nafasi ya mwenyekiti wa mtaa au kijiji ambayo itashirikisha wanachama wote wa matawi kitafanyika Oktoba 19 hadi  Oktoba 20, 2019.

Amesema baada ya kura za maoni katika matawi, kamati za siasa za halmashauri kuu za matawi zitajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za halmashauri kata.

Amesema Oktoba 27 hadi 28, 2019 kamati za siasa za halmashauri kuu za wilaya zitafanya uteuzi wa mwisho wa wanachama watakaogombea uenyekiti wa mtaa, ujumbe wa kamati ya mtaa, uenyekiti wa kijiji na ujumbe wa halmashauri ya kijiji.