CCM yawasamehe, yawaonya Nape, Ngeleja na January

Muktasari:

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imewasamehe wabunge wake watatu; January Makamba (Bumbuli), Nape Nnauye (Mtama) na William Ngeleja wa Sengerema kwa tuhuma zilizozidhalilisha chama na kuwaonya endapo wakirudia watachukuliwa hatua kali.

Mwanza. Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimewasamehe wabunge wake watatu juu ya tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.

Pamoja na kuwasamehe, imewaonya wabunge hao, January Makamba (Bumbuli), Nape Nnauye (Mtama) na William Ngeleja wa Sengerema kutorudia makosa hayo.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Desemba 13, 2019 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imesema hayo yamefikiwa katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.

Polepole amesema halmashauri hiyi imepokea, kujadili na kuridhia kwa kauli moja taarifa ya kamati ya usalama na maadili juu ya uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli wa kuwasamehe wanachama walioomba radhi kwake baada ya kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma.

“Kikao cha halmashauri kuu kimewataka wanachama hao kujirekebisha na kutorudia makosa yao ama sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama ikiwamo kufukuzwa uanachama,” amesema Polepole

Wabunge hao kwa nyakati tofauti walimwomba msamaha Rais Magufuli ambaye aliwasamehe baada ya sauti zinazodaiwa kuwa zao kusambaa mitandaoni wakizungumzia masuala ya kisiasa hususan ndani ya CCM.