VIDEO: Chadema yaahidi kuimarisha ulinzi mipakani

Saturday October 17 2020

Kigoma. Mgombea mwenza kwa tiketi ya Chadema, Salum Mwalimu amesema chama hicho kikiibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 kitaimarisha ulinzi wa mipakani kwa kutumia zaidi teknolojia na kuwaongezea uwezo askari wa jeshi la polisi.

Mwalimu ameeleza hayo leo Jumamosi Oktoba 17, 2020 katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Kumsenga jimbo la Muhabwe mkoani Kigoma.

Huku akieleza jinsi polisi wanavyofanya kazi nzuri  licha ya changamoto zilizopo amesema, “Chadema tunasema tutaimarisha sana ulinzi wa mipaka yetu hasa kwa kutumia teknolojia ili kutokuwa na askari wengi,  pia kutokuwa na mchanganyiko wa wageni na wenyeji, tutawaongezea weledi askari wetu kuweza kutambua kwa wepesi wageni.”

Amesema Chadema itaweka utaratibu maalumu wa kuhakikisha kila raia anafahamika kwa urahisi zaidi ili ahakikishiwe usalama wake na ulinzi kwani kuna changamoto kubwa ya wageni na wenyeji katika mikoa ya mipakani.

"Chadema tunaamini jeshi letu litafanya kazi kwa weledi, utaalamu na sayansi ya hali ya juu tofauti na ilivyo sasa. Maeneo ya mipakani OCD hatakiwi kutumia gari bovu inabidi awe na helkopta kudhibiti uingiaji sio kusubiri watu waingie halafu mtumie nguvu kuwachambua hali ambayo inaumiza na wenyeji," alisema Mwalimu.

 

Advertisement
Advertisement