Chadema yatoa ratiba ya uchaguzi wa viongozi- Video

Chadema yatoa ratiba ya uchaguzi wa viongozi- Video

Muktasari:

  • Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kinachoongozwa na Freeman Mbowe kimetangaza ratiba ya uchaguzi wake ngazi ya Taifa.

Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimetangaza ratiba ya uchaguzi wa viongozi wake ngazi ya Taifa.

Mchakato huo unaanza na uchukuaji na urejeshaji fomu kuanzia leo Jumatatu Novemba 18 hadi Novemba 30, 2019 huku mkutano mkuu ukifanyika Desemba 18, 2019.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji akizungumza na wanahabari makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam amesema uchaguzi huo utaanza kwa kuchagua viongozi ngazi ya mabaraza na kufuatiwa na viongozi wakuu wa chama ngazi ya Taifa.

"Baada ya kazi ya uchukua na kurejesha fomu kutakuwa na vikao mbalimbali vitakavyoanza Desemba 7, 2019 ambapo kamati kuu itakutana kuchuja na kupitia majina ya wote walioomba nafasi mbalimbali kwaajili ya uteuzi wa awali," amesema Dk Mashinji

Amesema baada ya kupitia majina ya wote walioomba, Desemba 8, 2019 kamati tendaji ya baraza la vijana na wazee watakutana na kufuatiwa na mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa mabaraza hayo Desemba 9, 2019.

Dk Mashinji amesema Desemba 10, 2019 kamati tendaji ya baraza la wazee na vijana itakutana ambapo ni vikao vinavyofanyika kufuatiwa na mkutano mkuu.

"Desemba 11, 2019 kamati tendaji ya baraza la wanawake watakaa na kufuatiwa na mkutano mkuu Desemba 12, 2019.

Aidha Dk Mashinji amesema baada ya chaguzi za mabaraza yote Desemba 16, 2019 kamati kuu ya chama itakutana kufanya uteuzi wa viongozi ngazi ya Taifa.

"Desemba 17, 2019 utafanyika mkutano wa baraza kuu la chama ambapo watafanya uteuzi wa mwisho kwaajili ya kupeleka majina ya wagombea kwenye mkutano mkuu wa chama Desemba 18, 2019," amesema

"Katika nafasi za mabaraza uchaguzi utakaofanyika ni mwenyekiti, makamu wenyeviti wawili bara na Zanzibar, katibu mkuu, mweka hazina, wajumbe watano na wajumbe 20 watakaokuwa wawakilishi wa Baraza kuu," amesema.