Chadema yazungumzia wagombea virusi uchaguzi mkuu 2020

Muktasari:

 Wimbi la wabunge na madiwani kujitoa vyama vya upinzani na kurejea CCM lilikitikisa zaidi Chadema kuanzia mwaka 2017 ambako wabunge wake saba walikihama chama hicho huku Idadi ya madiwani wake zikizidi 140.

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoa Kilimanjaro nchini Tanzania kimesema hakiko tayari kupokea wagombea aliowafananisha na virusi, katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na Rais.

Hata hivyo, haikuwekwa wazi kama wanaolengwa ni wale waliopewa dhamana na chama hicho uchaguzi mkuu 2015, lakini miaka miwili baadaye wakajitoa Chadema na kurejea chama tawala.

Wabunge tisa wakiwamo wawili wa CUF na saba wa Chadema na zaidi ya madiwani 140 wa vyama hivyo viwili walirejea CCM na wengi wao wakisema ni kwenda kumuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli.

Msimamo huo wa kukataa wagombea virusi umetangazwa leo Jumanne Januari 7, 2020 na mwenyekiti wa chama hicho, Michael Kilawila ambaye alisema yuko tayari kujiuzulu kuliko kupokea mgombea anayetafuta fursa kwa fedha.

Kilawila aliyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa Baraza la Wanawake (Chadema) mkoa Kilimanjaro uliokuwa na lengo la kutoa mwelekeo wa mwaka wa uchaguzi mkuu 2020.

“Tunapojiandaa kwenda kwenye uchaguzi mkuu, kila mtu kwenye mkoa huu atakula alipopeleka mboga. Yaani wewe unataka kuwa ubunge utatuonyesha kazi uliyofanya,” almesisitiza Kilawila.

“Niko tayari kujiuzulu nafasi yangu ya mwenyekiti wa mkoa kuliko kuletewa virusi ambavyo havijafanya kazi. Tumeelewana? Yaani wengine watoke jasho wewe uje tu utake kugombea,” amehoji.

“Wewe mwenzako akaandikishe Chadema ni msingi, akalale nje ya ndoa yake halafu mtu aje na senti zake halafu tumuidhinishe kuwa mgombea kupitia chama chetu. Hiyo haitakaa itokee,” amesema.

Kilawila amesema bahati nzuri katiba ya Chadema imebadilishwa na uamuzi wote wa kupitisha wagombea utafanywa na vikao vya mkoa na kuwaeleza kuwa “safari hii tunanyoana hapa hapa”

Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Bawacha mkoa Kilimanjaro, Grace Kiwelu ametangaza mikakati mitatu ambayo itafanywa na baraza lake kwa lengo la kupata ushindi wa jumla wa chama hicho.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha kazi ya Chadema ni msingi na kuhamasisha wanawake wengi kujisajili katika daftari la chama na kuratibu mafunzo kwa wanawake na kuwahamasisha kugombea.

“Zoezi la Chadema ni msingi tulilolifanya kuanzia mwanzo mwa mwaka jana ndio roho na uimara pekee wa chama chetu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 wa Rais, wabunge na Madiwani,” amesema Kiwelu.

“Mwaka huu (2020) tuliusubiri kwa hamu kubwa. Ni mwaka wa kazi kuu ya kiutume ya kumkomboa mwanamke na kuikomboa nchi yetu. Twendeni kazini. Watanzania wanatuunga mkono,” amesisitiza.