Chokala: Nitaendesha nchi kwa reli, bandari

Balozi Patrick Chokala, akizungumza na waandishi  jijini Dar es Salaam jana, wakati alipokuwa akitangaza nia yake ya kuomba kuteuliwa  kuwa mgombea urais kupitia CCM. Kushoto ni  Mchungaji Ibrahim Chegere.
Na Mpiga Picha Wetu

Muktasari:

Balozi huyo mstaafu na mwandishi wa habari mkongwe, anaungana na makumi ya wanaCCM waliokwishajitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa katika uongozi wa nchi na anatarajiwa kwenda Dodoma kesho kudhihirisha nia yake kwa kuchukua fomu.

Dar es Salaam. Balozi Patrick Chokala (67), amejitokeza na kutangaza azma yake ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM akiahidi kusimamia uchumi wa Taifa kupitia bandari na reli.

Balozi huyo mstaafu na mwandishi wa habari mkongwe, anaungana na makumi ya wanaCCM waliokwishajitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa katika uongozi wa nchi na anatarajiwa kwenda Dodoma kesho kudhihirisha nia yake kwa kuchukua fomu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), Balozi Chokala alisema ametafakari kwa muda mrefu kabla ya kufikia uamuzi wa kujitosa katika kinyang’anyiro hicho huku akijigamba kwamba wingi wa watangaza nia waliojitokeza haumtishi.

Alisema anaamini kuwa anazo sifa na kila sababu ya kugombea urais kwa sababu ana uzoefu wa miaka 13 serikalini na nje ya nchi.

Alisema amejipanga vyema kuwatumikia wananchi endapo atapata ridhaa hiyo na kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa kukuza uchumi kupitia sekta hizo mbili za bandari na reli.

“Uchumi wa nchi yoyote unategemea bandari na reli, licha ya nchi yetu kuboresha hivi vitu, lakini ufanisi wake ni mdogo. Hivyo nikichaguliwa nitahakikisha naboresha miundombinu ya bandari,” alisema.

Alisema hata reli iliyopo inahitaji kufanyiwa marekebisho ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi na kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi. Alisema pia atasimamia ulinzi wa barabara ili ziwe na hadhi badala ya kutengenezwa mara kwa mara.

“Reli hii inayotumika sasa hivi ipo tangu enzi za mkoloni, unafikiri itaweza kufanya kazi vizuri? alihoji na kuendelea: “Ndiyo maana nasema nikiingia madarakani nimepanga kuiboresha kwa kuijenga reli ya umeme mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ili kurahisisha usafiri kwa wananchi kiasi cha mtu kuweza kwenda na kurudi Mwanza kwa siku moja kama vile nchi za Ulaya zinavyofanya,” alisema Balozi Chokala.

Alisema sababu nyingine iliyomsukuma awanie nafasi hiyo ya urais ni kuona Tanzania yenye haki, upendo na utajiri.

“Leo (jana) natamka rasmi kuwa natangaza nia ya kugombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi na naomba ridhaa ya chama changu kinipitishe kwa sababu nina uzoefu na Ikulu. Nimekaa serikalini kwa miaka 13, hivyo siyo mgeni na eneo hili, hata nikiamua kupiga mluzi Ikulu nasikika,” alisema Chokala ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa balozi, alikuwa Mwandishi wa Habari wa Rais.

Akizungumzia ufanisi wa bandari, Balozi Chokala alitolea mfano wa Misri ambayo alisema asilimia 75 ya mapato yake, yanatokana na matumizi ya bandari na kusema hata hapa nchini, itawezekana endapo kutapatikana kiongozi bora na madhubuti.

“Tujiulize, tunapata kiasi gani kwenye Bandari Dar es Salaam? Zaidi ya hapo, tunazo bandari nyingine ambazo bado hazijatumika kikamilifu mfano Tanga, Bagamoyo, Lindi na Mtwara,” alisema Balozi Chokala ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Urusi kwa miaka sita.

Alisema tatizo la kutokuwapo kwa miundombinu ya kutosha ikiwamo ya barabara na reli, kunalifanya Taifa likose mapato na hivyo kushindwa kujiendesha kwa kujitegemea.

Mara ya pili kutangaza nia

Alisema kuwa hii ni mara ya pili kwake kutangaza nia ya kutaka kuwania urais. Mwaka 2005 alifanya hivyo wakati akiwa Balozi nchini Urusi na kushindwa.

“Nakumbuka mwaka 2005 tulijitokeza watu 11 lakini mwaka huu ni tofauti. Lakini hali hii hainitishi maana wote waliojitokeza nawajua utendaji wao wa kazi wakiwamo mawaziri. Ni imani yangu kuwa nitakuwa mmoja wa watakaoipeperusha bendera ya CCM katika urais,” alisema Balozi Chokala na kuongeza: “Mimi kwenda Ikulu ni kama narudi nyumbani kwani nilishawahi kufanya kazi hapo awali. Nawahakikishia wananchi nitaziboresha huduma muhimu za jamii ikiwamo usafiri, makazi ya wazee sanjari na matibabu.”

Alipoulizwa ni mgombea yupi anayemdhania kwamba anaweza kuchaguliwa ambaye atasimama kumpigia kampeni endapo hatapitishwa na chama chake, Balozi Chokala alisema haoni mgombea tishio kwake.

“Hawa waliojitokeza ndiyo wajiandae kunisaidia kupiga kampeni za urais, kwani nina uhakika nitaibuka namba moja,” alisema.

Balozi Chokala ambaye kabla ya kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais alikuwa Mwandishi wa iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), alisema licha ya bandari na reli, Tanzania ina utajiri wa madini, hivyo akichaguliwa atahakikisha rasilimali hizo zinatumika ipasavyo kuwanufaisha wananchi.

“Nilipokuwa nafanya kazi ubalozini Moscow, wenzetu walikuwa wanatushangaa pindi tunapoomba misaada, wakati nchi yetu imebarikiwa kuwa na utajiri wa madini ambao ukiwekwa mikakati mizuri unaweza kutupa maendeleo,” alisema Balozi.

Alisema Serikali atakayoiunda itasimamia masilahi ya Watanzania, ikiwamo misaada mbalimbali inayotolewa na wahisani kwa lengo la kuboresha miundombinu ya nchi.

“Nilifanya ziara Japan nikakutana na mkurugenzi wa Jica ambaye alinilalamikia kuwa baadhi ya misaada inayotolewa na wahisani inaishia mifukoni mwa wakubwa…. Hali hii ndiyo inayofanya nchi ishindwe kutimiza mipango yake,” alisema.

Balozi huyo alisema atahakikisha wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga wanatengewa maeneo maalumu kwa ajili ya kufanya biashara zao kwa amani na utulivu ili kujiingizia kipato.

Kuongeza bajeti ya kilimo

Akizungumzia kilimo, Balozi Chokala alisema atahakikisha wizara husika inapewa kipaumbele kwa kutengewa bajeti ya kutosha ili kuwainua wakulima wadogo na sanjari kuwatafutia masoko ya nje ya nchi lengo likiwa kukuza pato la Taifa.

“Nitahakikisha naviboresha viwanda vikubwa na vidogo hususan vyenye kulenga matumizi ya malighafi ya kilimo ili kuongeza ajira ya vijana,” alisema Balozi Chokala.

Vipaumbele vingine

Mbali ya bandari, reli na kilimo, Balozi Chokala alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kipato cha kati na kuukuza kwa kupambana na umaskini, kuimarisha ukuaji wa viwanda, uchukuzi na utalii.

Uchukuaji wa fomu Dodoma

Balozi huyo anatarajia leo kuchukua fomu mkoani Dodoma na kuanza ziara ya kutafuta wadhamini katika mikoa mbalimbali kwa kutumia magari ya kawaida akisema atakuwa tofauti na watangaza nia waliomtangulia.

“Kesho (leo) natarajia kuchukua fomu mjini Dodoma, nina uhakika nitapata wadhamini wa kutosha na msafara wangu wa kuzunguka kuwatafuta watu hawa utakuwa wa kawaida kwa maana ya magari, sina haja ya kutumia ndege na msafara wangu utakuwa wa kipekee,” alisema.