VIDEO: DC Jokate atoa somo usimamizi wa fedha za maendeleo

Saturday October 12 2019

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Kisarawe. Mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani nchini Tanzania, Jokate Mwegelo amewataka viongozi katika wilaya hiyo kusimamia kwa ufanisi fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Jokate ameyasema hayo jana Ijumaa Oktoba 11, 2019 wakati akizindua vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kola ambayo ujenzi wake ulikwenda sambamba na ujenzi wa ofisi ya walimu na matundu manne ya vyoo.

Alisema kwa wakati huu Kisarawe inahitaji viongozi wazalendo watakaoonyesha uzalendo kwa kusimamia vyema fedha zinazotolewa na serikali kwa lengo la kufanikisha miradi mbalimbali.

“Ni lazima tujue ni kwa nini hatujafikia asilimia 100 ya utekelezaji wa miradi wakati fedha zote zimeingia kwenye akaunti. Tunahitaji kuwa na viongozi watakaosimamia fedha na rasilimali zinazotoka serikalini na watakaokuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo,” alisema

Jokate aliwataka wanafunzi na walimu wa shule hiyo kutumia vyema majengo waliyokabidhiwa katika kuhakikisha yanakuwa chachu katika kuinua sekta ya elimu wilayani Kisarawe. 

“Tuyatumie vizuri madarasa haya, tuyatunze tukihakikisha watoto wanasoma na kiwango cha elimu kinakuwa, tumedhamiria kupiga hatua na hakika kwa pamoja tutafanikisha hilo,”

Advertisement

Hatua hiyo ni utekelezaji wa kampeni ya Tokomeza Ziro inayoratibiwa na mkuu wa wilaya huyo inayolenga kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.

Advertisement