DC Sabaya aagiza Halmashauri ikatiwe umeme

Muktasari:

  • DC Sabaya alifikia uamuzi huo baada ya Halmashauri hiyo kutolipa bili ya umeme ya soko la Bomang'ombe na kusababisha wakatiwe umeme

Hai. Mkuu wa wilaya ya Hai (DC) mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania,  Lengai Ole Sabaya ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuikatia umeme Halmashauri ya wilaya ya Hai hadi watakapolipa bili ya Sh262,000 wanazodaiwa katika soko la Bomang'ombe.

Sabaya alitoa maagizo hayo leo Jumatano Septemba 25, 2019 alipofanya ziara katika soko hilo na kukuta wafanyabiashara wamekatiwa umeme katika vibanda vyao vya biashara kutokana na Halmashauri kutolipa deni hilo.

Pamoja na mkurugenzi wa Halmashauri aliyekuwepo katika mkutano huo, Yohane Sintoo kuwaomba radhi wananchi, lakini Sabaya akaagiza Halmashauri ikatiwe umeme kisha Tanesco irudishe umeme katika soko hilo.

Sabaya amesema haiwezekani Halmashauri wanakusanya ushuru kwa wafanyabiashara hao kila mwezi, lakini yenyewe inashindwa kulipa deni la umeme kwa miezi miwili.

Amemwagiza Meneja wa Tanesco wilaya ya Hai, Theodory Hilal kukata umeme ofisi za Halmashauri na kwamba kibali cha kuurejesha atakitoa yeye baada ya kuona risiti za malipo za kulipwa deni hilo.