DIT watakiwa kuboresha mitalaa ya elimu

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Elias Kwandikwa

Muktasari:

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Elias Kwandikwa ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuboresha mitalaa ya elimu ili kuwajengea uwezo wanafunzi wake kushindana kimataifa.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Elias Kwandikwa ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuboresha mitalaa ya elimu ili kuwajengea uwezo wanafunzi wake kushindana kimataifa.

Kwandikwa ametoa wito huo leo Alhamisi Desemba 12, 2019  jijini Dar es Salaam alipomuwakilisha Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa katika mahafali ya 13 ya chuo hicho.

Wanafunzi 1,071 wamehitimu katika ngazi za astashahada, stashahada na shahada za awali na uzamili.

Amesema Serikali imewekeza katika mafunzo ya ufundi ili kuibua wataalamu wengi wa teknolojia hasa wakati huu wa jitihada za kujenga uchumi wa viwanda.

"DIT endeleeni kuboresha mitaala ili kuwaongezea wanafunzi wenu nguvu ya ushindani kimataifa. Teknolojia inakua kila siku, lazima  mbadilike kulingana na mabadiliko ya teknolojia," amesema Kwandikwa.

Waziri huyo amesema nchi zilizowekeza kwenye teknolojia zimepiga hatua kubwa kiuchumi huku akitolea mfano China na Japan.

Amesema kwa sababu hiyo Serikali nayo imeanza kuwekeza kwenye elimu ya ufundi ili kupata wataalamu wengi katika eneo hilo.

Kwandikwa amewataka wahitimu hao kwenda kufanya ubunifu na kujiajiri wenyewe kwa sababu utaalamu wao unahitajika katika jamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Profesa Appolonia Pereka amesema chuo hicho kinatekeleza mradi wa kuboresha mafunzo ya ufundi yanayohitajika katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema mradi huo utakaogharimu Sh74 bilioni umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Mwenyekiti huyo amebainisha changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa ruzuku ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo kutoka serikalini.

Mkuu wa Taasisi ya DIT, Profesa Preksedis Ndomba amesema wameingia mikataba zaidi ya 27 na viwanda na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Amesema ushirikiano huo umewafanya wanafunzi wa taasisi hiyo kuwa mahiri katika fani zao kwa sababu wanapata fursa ya kwenda kujifunza kwa vitendo na kuona jinsi kazi zinavyofanyika kiuhalisia.