DPP awaonya watakaovuruga amani Tanzania

Mkurugenzi wa mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga

Muktasari:

Mkurugenzi wa mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amesema yeyote mwenye lengo la kuvuruga amani ya nchi  atashughulika bila kujali dini,  jinsia wala cheo chake.

Mafinga. Mkurugenzi wa mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amesema yeyote mwenye lengo la kuvuruga amani ya nchi  atashughulika bila kujali dini,  jinsia wala cheo chake.

Biswalo ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 23, 2020 wakati akizindua ofisi ya Taifa ya mashtaka wilaya ya Mufindi iliyopo mjini Mafinga, akisisitiza kuwa jukumu la amani ya nchi ni la kila Mtanzania.

Amesema lengo kuu la kufungua ofisi hiyo ni pamoja na kuondoa  malalamiko ya uvunjifu wa amani.

“Ni vizuri kulinda amani tuliyonayo kwa sababu machafuko yakitokea tutaenda wapi? Nchi nyingi zinataka tuharibikiwe kwa sababu wao wameshaharibikiwa, hivyo ni vizuri taratibu  na shEria za nchi tulizojiwekea tuzifuate ili tuweze kupata haki, amani na usalama na nchi iweze kupata maendeleo,” amesema Biswalo.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William amewataka wananchi kuitumia ofisi hiyo kupata haki na kulinda amani ya wilaya ya Mufindi na mji wa Mafinga.

“Ofisi hii itawasaidia wananchi kuwa na utawala bora na kesi kuendeshwa kwa haki na kuondoa malalamiko kwa wananchi katika ukiukwaji wa haki kwa wananchi na uvunjifu wa amani, ”amesema Jamuhuri