Daktari mbaroni kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno

Muktasari:

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia daktari wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Albert Rugai (65) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Ester Kondo (42).

Kibondo. Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia daktari wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Albert Rugai (65) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Ester Kondo (42).

Daktari huyo aliyekuwa katika kambi ya wakimbizi ya Nduta baada ya kufanya mauaji hayo yanayodaiwa kuwa chanzo chake ni wivu wa mapenzi, naye alijaribu kujiua kwa kunywa sumu.

Akizungumza leo Jumatano Januari 15, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno amesema mauaji hayo yametokea Januari 12, 2020 wilayani Kibondo.

Amesema wakiwa nyumbani daktari huyo alimpiga Ester na nyundo kichwani, “ubongo ulitoka nje na alivuja damu nyingi. Alikufa akiwa nyumbani.”

Amesema Rugai baada ya kufanya mauaji hayo alikunywa sumu ili kujiua.

“Yupo hospitali akipatiwa matibabu na atakapopona atafikishwa mahakamani. Niwashauri wananchi waache kujichukulia sheria mkononi. Kama unaona mpenzi wako ana shida achana naye utafute mwingine. Usijitafutie matatizo ona huyu mzee na umri wake anakwenda kufia jela," amesema Ottieno.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Kibondo, Mathias Bwashi amekiri  kupokea mwili wa mwanamke huyo na mtuhumiwa anayeendelea kupatiwa matibabu.