Dar es Salaam tishio kwa ajali za barabarani

Tuesday April 30 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Uwezekano wa kufa kwa ajali za barabarani ni mkubwa zaidi katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake kuliko eneo lolote nchini, takwimu za polisi zimeonyesha.

Jiji lina maeneo korofi kwa ajali za barabarani ikiwemo barabara ya Mandela, Morogoro na Kawawa zimetajwa kuwa na matukio mengi ya ajali.

“Hii barabara ya Mandela tunashuhudia ajali nyingi kila siku, hapa katika mataa ya Tabata mpaka kuelekea Buguruni ajali haikosekani, nyingi ni za waenda kwa miguu na bodaboda,” alisema mfanyabiashara ya chakula eneo la Tabata Matumbi, Amina Juma alipoulizwa kuhusu matukio ya ajali katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi, asilimia 53 ambayo ni zaidi ya nusu ya ajali zilizotokea nchini kati ya Januari na Machi mwaka 2019, zilitokea jijini Dar es Salaam.

Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani, zimeonyesha kati ya ajali 776 zilizotokea nchini kwa kipindi hicho, 416 zilitokea Dar es Salaam.

Ajali hizo ni jumla ya zote zilizotokea katika mikoa 30 kote Tanzania Bara, huku mikoa mitatu ya kipolisi jijini Dar es Salaam (Kinondoni, Ilala na Temeke) ikichangia zaidi ya asilimia 53 ya ajali zote.

Advertisement

Takwimu hizo zinaonyesha Kinondoni na Ilala ndiyo mikoa inayoongoza kwa ajili kwani pekee zilikuwa na ajali 384 namba ambazo zinazidi zile za mikoa mingine zikikusanywa pamoja.

Akitoa takwimu hizo Kamanda wa Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani nchini Fortunatus Muslimu alisema Kinondoni inaongoza kwa ajali ikilinganishwa na mikoa mingine 29 Tanzania Bara.

Alisema mkoa huo wa kipolisi unaongoza kwa tofauti ya ajali 213, kati ya ajali 776 zilizotokea katika mikoa mbalimbali.

“Ilala na Kinondoni pekee zimechukua ajali 384 huku mikoa mingine 27 ikiwa na ajali 360 wakati huohuo mkoa wa Temeke ukiwa na ajali 32 pekee, hii inaonyesha namna jiji la Dar es Salaam lilivyo na matukio mengi ya ajali ikilinganishwa na mikoa mingine ya kipolisi,” alisema Kamanda Muslimu.

Kwa mujibu wa Kamanda Muslimu ajali hizo zilichangia majeruhi 735 na vifo 335.

Hata hivyo Muslimu alisema ajali kwa sasa zimepungua ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018.

“Januari na Machi mwaka 2018, jumla ya ajali za barabarani ilikuwa ni 1,183, huku kwa Dar es Salaam peke yake ikichangia jumla ya ajali 653, hapa utaona ni namna gani jiji hili linachangia ajali nyingi kulinganisha na maeneo mengine ya nchi,” alisema Muslimu.

Hata hivyo ajali za bodaboda ndizo zilizorekodiwa zaidi katika hospitali na vituo vya afya ukilinganisha na zile zitokanazo namagari jijini Dar es Salaam.

Ajali hizo zimekuwa zikiigharimu Serikali katika upande wa matibabu, takwimu zinaonyesha kati ya majeruhi 22,836 waliofanyiwa upasuaji kitengo cha dharura Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) mwaka 2015-2018, asilimia 70 walikuwa ni majeruhi wa bodaboda.

Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na magonjwa ya ajali (Moi) Kennedy Nchimbi aliliambia Mwananchi kuwa takwimu walizonazo zinaonyesha idadi ya majeruhi mwaka 2015/16 ilikuwa wagonjwa 7,884 na mwaka 2016/17 ilipungua kufikia 6,669 na kwa mwaka 2017/18 iliongezeka hadi kufikia 8,283 na kufanya jumla ya wagonjwa waliohudumiwa kufikia 22,836 ambapo asilimia 70 walikuwa wa ajali za bodaboda.

Alisema wagonjwa wengi wanaumia maeneo mchanganyiko sehemu yoyote ambayo itagongwa kwa muda huo, kwa kuwa pikipiki ni chombo kilicho wazi hivyo ni rahisi kuumia mguu, kiuno, kifua na maeneo mengineyo ya mwili, licha ya wanaoumia vibaya kichwani hutokana na kutovaa helment.

Kamanda Muslimu alipoulizwa kuhusu nini kinafanyika kupunguza ajali hizo, alisema kwa sasa wana mikakati mbalimbali wanayoifanya ili kupunguza ajali hizo.

“Tuna mikakati mbalimbali tunayoitumia ili kuondokana na ajali ikiwemo kutoa elimu, operesheni mbalimbali ikiwemo nyakuanyakua, kuna suala la usimamizi wa sheria na tumekwenda mbali zaidi kwa kushirikisha wadau na matumizi ya teknolojia ikiwemo kufungwa kwa kamera barabarani kwa kushirikiana na wizara ya ujenzi na hili litafanyika kote nchini,” alisema Muslimu.

Advertisement