Dawa bora zaidi katika kufubaza VVU sasa rasmi

Wednesday December 11 2019

Mtafiti Kennedy Ngowi kutoka Kilimanjaro

Mtafiti Kennedy Ngowi kutoka Kilimanjaro Christian Research Institute (ICT) akipongezwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile mara baada ya kushinda tuzo wakati wa mkutano wa 20 wa kimataifa wa masuala ya HIV na magonjwa ya zinaa ICASA2019 uliofanyika nchini Rwanda. Ngowi alishinda tuzo hiyo baada ya kutengeneza huduma ya mtandao ‘mobile health’ kuelimisha masuala ya HIV na uzazi wa mpango. Na Mpiga Picha Wetu 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ni rasmi sasa. Tanzania imeingia katika matumizi ya dawa mpya na yenye ufanisi zaidi katika kufubaza virusi vya Ukimwi iitwayo Dolutegravir (DTG).

Kwa hatua hiyo, Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi 82 duniani zenye kipato cha chini na kati zilizoanza matibabu ya VVU kwa kutumia DTG.

Akizungumza na Mwananchi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema kuna mabadiliko ya dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi.

Alisema dawa hiyo inatumika katika mseto na dawa nyingine za tenofovir 300mg/, lamivudine 300mg/ na Dolutegravir 50mg (yaani TLD kwa kifupi)

“Dolutegravir ni dawa mpya ambayo imeanza kutumika nchini badala ya ile ya awali ya efavirenzi,” alisema Dk Ndugulile.

Alisema dawa hiyo inapunguza maambukizi, lakini akaonya kuwa wagonjwa wanashauriwa kutoacha kutumia dawa na kinga dhidi ya VVU.

Advertisement

“Kwa sisi Tanzania, matumizi ya dawa hii tuliyaanza Machi mwaka huu, lakini tunashauri watu wasiache kutumia dawa na kinga hata kama wamefubaza VVU,” alisema.

Dk Ndugulile alitoa onyo hilo kutokanas na taarifa kuwa mtu akianza kutumia dawa hiyo, virusi havionekani na hawezi kuambukiza mwingineu hata akifanya mapenzi bila kinga.

Wataalamu waliozungumza na Mwananchi wameeleza kuwa dawa hiyo ina uwezo wa kufubaza virusi vya Ukimwi kwa haraka.

Kuhusu TLD

Mtaalamu kutoka Shule ya Famasia ya Chuo Kikuu cha Sayansi Muhimbili (Muhas), Nelson Masotta alisema awali dawa ambayo ilitumika ilikuwa TLE.

“Hii ni muunganiko wa dawa tatu tenofovir, lamivudine na efavirenz kwa kifupi TLE. Hiyo dawa ya mwisho imeonekana kuwa na madhara au maudhi (side effects) madogomadogo kwa muda sasa,” alisema Masotta.

Alisema kutokana na kuwepo kwa mapungufu katika efavirenz na kusababisha usumbufu kwa wagonjwa wakati wa matibabu yao, ilipendekezwa dawa nyingine.

“Katika muendelezo wa kutafuta tiba bora zaidi, ndipo ikaonekana dawa nyingine ya Dolutegravir inaweza pia kuunganishwa na dawa zile mbili za mwanzo na kuleta matokeo mazuri kwenye tiba.”

Masotta alisema Dolutegravir ilikuwepo nchi nyingine, hasa zilizoendelea, lakini hapa nchini ni mpya.

“Kwa hiyo mchanganyiko unaotumika kwa sasa ni wa tenofovir+lamivudine+Dolutegravir (TLD),” alisema.

Inaweza kutumiwa na wote

Kwa kuzingatia ushahidi mpya uliotathimini faida na hatari, Julai 22, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza matumizi ya DTG kama njia ya kwanza na ya pili ya matibabu inayopendekezwa kwa watu wote.

WHO walisema dawa hiyo itaweza kutumiwa na watu wote, wakiwemo wanawake wajawazito na wale wenye uwezekano wa kupata ujauzito.

Utafiti wa awali ulionyesha kuna uwezekano wa kuwepo kwa uhusiano kati ya dawa hiyo ya DTG na tatizo la uti wa mgongo na ubongo ambalo linasababisha watoto kuzaliwa na matatizo kama vile tatizo la mgongowazi pindi mwanamke anapopata ujauzito akiwa katika matumizi ya dawa hiyo.

Kasoro hiyo iliripotiwa Mei mwaka 2018 kutokana na utafiti uliofanyika nchini Botswana na kukuta matukio manne ya matatizo hayo kati ya wanawake 426 ambao walipata ujauzito wakati wakimeza dawa za DTG.

Kutokana na utafiti huo wa awali, nchi nyingi zilishauri wanawake wajawazito na wanawake wenye uwezekano wa kubeba ujauzito, kumeza dawa za efavirenz badala ya DTG.

Hata hivyo, DTG ni dawa ambazo zimeonyesha ufanisi zaidi, rahisi kumeza na zina madhara madogo kuliko dawa nyingine ambazo zinatumika hivi sasa.

Advertisement