Dawa za figo zapungua Muhimbili, wagonjwa katika wakati mgumu

Dar es Salaam. Wagonjwa waliopandikizwa figo wanalazimika kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ili kupata dawa zao, baada ya kuadimika sehemu nyingine.

Awali wagonjwa hao walikuwa wakipewa dozi ya muda mrefu iliyowawezesha kutumia bila kurudi hospitali mara kwa mara. Wagonjwa hao hupata matibabu hayo katika maisha yao yote tangu wanapokuwa wamepandikizwa kiungo hicho ili kuuwezesha mwili ukubaliane na kiungo kipya mwilini.

Mwezi Agosti, MNH ilieleza jinsi ilivyookoa Sh3.5 bilioni tangu kuanza kutoa huduma ya upandikizaji figo Novemba, 2017.

Ofisa uhusiano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha alisema wagonjwa 47 wameshapandikizwa figo kwa gharama yaSh1.1 bilioni.

Wakati Aligaesha akieleza hayo, daktari bingwa na mkuu wa kitengo cha figo, Jackline Shoo alisema hadi siku hiyo walikuwa na wagonjwa zaidi ya 300 wanaopatiwa huduma ya kusafishwa damu na karibu nusu yao wanahitaji kupandikizwa figo.

Kila baada ya wiki mbili, Prisca Mwingira ambaye ni mwalimu anayeishi Morogoro mjini analazimika kusafiri kuja jijini Dar es Salaam kupata vidonge vya Tacrolimus ili kuudhibiti mwili usije ukaikataa figo iliyopandikizwa miaka miwili iliyopita.

“Awali nilikuwa nikisafiri mara moja hadi miezi mitatu kuja Dar es Salaam, lakini si siku hizi,” alisema Prisca ambaye ni mgonjwa wa kwanza wa Tanzania kupandikizwa figo MNH. katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Si peke yake, yupo pia Pegi Lunyili aliyefanyiwa upandikizaji wa figo nchini India, ambaye anasema safari za Muhimbili zinaathiri kazi zake na kuongeza gharama.

“Limekuwa tatizo kwa miezi mitatu sasa. Inakuwa ngumu hasa ninapoomba ruhusa ya kutoka kazini kila mara, kwani nalazimika kuacha kazi nyingi ili kupata matibabu. Lakini naamini hili linaweza kupatiwa ufumbuzi,” Lunyili.

Mgonjwa ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi alisema kwamba amewatafuta wagonjwa wenzake na kwenda kuhoji uongozi wa hospitali hiyo sababu ya kukosekana kwa dawa kama ilivyokuwa awali.

“Niliambiwa kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi lakini mpaka sasa bado tunapata shida ya kuja hospitalini hapa mara kwa mara,” alisema mtu huyo anayeishi Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

MNH walisema tatizo la kupungua kwa dawa hizo lilianza Septemba mwaka huu na kwamba wanatafuta ufumbuzi.

“Tulikuwa na dawa za Julai hadi Septemba, lakini hivi karibuni tumekuwa na changamoto ya upatikanaji wake. Ndiyo maana tumeamua kutoa dozi ndogo kwa wagonjwa inayodumu kwa siku mbili hadi tatu hadi wiki moja. Ninakubali ni tatizo hasa kwa wagonjwa wanaosafiri umbali mrefu,” alisema Aligaesha akikiri tatizo hilo.

Aliongeza, “Tunafanya kazi usiku kucha kuhakikisha tatizo hili linapatiwa ufumbuzi,” alisema Aligaesha bila kufafanua kwa undani jinsi changamoto ya ununuzi wa dawa hiyo ilivyo.