Diamond ashindwa kupanda Mlima Kilimanjaro, Steve Nyerere azitema Sh2 milioni

Muktasari:

Safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa wasanii mbalimbali pamoja na waandishi wa habari ilianza jana Jumamosi ambapo leo Jumapili baadhi yao wameanza kurudi kutokana na sababu kadhaa.

Moshi. Pamoja na majigambo aliyoyafanya ya namna atakavyoupanda Mlima Kilimanjaro, msanii wa filamu nchini Tanzania, Steve Nyerere amekuwa miongoni mwa wasanii watatu walioshindwa kutimiza ndoto hiyo.

Steve Nyerere aliungana na wasanii wengine jana Jumamosi Septemba 28, 2019 katika kuupanda mlima huo ambapo ni kampeni ya 'Kili Challenge Twenzetu Kileleni.'

Kampeni hiyo iliyoandaliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii n chini Tanzania, Dk Hamis Kigwangala akimshirikisha Miss Tanzania 2018, Elizabeth Makune kupitia kampeni yake ya 'Twenzetu Kutalii' ilizindiliwa rasmi jana Jumamosi.

Kampeni hiyo  imelenga kuhamasisha utalii wa ndani, ambapo zaidi watu 130 wakiwemo  wasanii walianza kuupanda mlima huo, safari itakayochukua siku sita.

Safari ya kuelekea mlimani ilianza saa 5:45 asubuhi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kumkabidhi bendera Waziri Kigwangala.

Hata hivyo, katika safari hiyo msanii Diamond Platnumz aliishia nusu ya safari ya kituo cha kwanza cha Mandara, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni  kutingwa na majukumu mengine.

 

Wasanii wengine walioshindwa kusonga mbele ni Steve Nyerere, Dogo Janja na JB ambao wenyewe wameshuka leo Jumapili.

Wasanii hao wamejikuta wakishindwa baada ya kuchoka na kuwaacha wengine wakiendelea na safari ambapo wanatarajia kulala  kituo cha pili cha Horombo.

Katika kuhakikisha anampa moyo Steve ili aendelee, msanii wa Bongofleva, MwanaFA aliahidi kumpatia Sh1 milioni msanii huyo kama atafanya hivyo, ambapo baadaye Waziri Kigwangala alimuongezea Sh1 milioni na mdau mwingine wa utalii  Sh500,000.

Pamoja na fedha hizo kufika Sh2.5 milioni,  Steve alizikataa na kurudia kituoni hapo Mandara leo asubuhi hivyo MwanaFA kuchukua Sh1 milioni yake ambayo alikuwa amekwisha kumpa azishike.

Akizungumzia hilo, Steve amesema hakuwa tayari kutoa uhai wake kisa Sh2.5 milioni kwani kwa namna alivyokuwa akisikia maumivu kwenye mwili wake ilikuwa ngumu kuendelea na safari hiyo.

"Hela na uhai kikubwa uhai bwana, asikuambie mtu na hata hivyo hizo hela mbona hata mimi ninazo kwa nini nijiumize," amesema Steve.

Kwa upande wake, Dogo Janja amesema walirudi kwa sababu ya kukabiliwa na majukumu mengine.

Naye JB amesema kupanda mlima Kilimanjaro sio kazi ndogo kama watu wanavyofikiria na kuongea kuwa ni kazi kubwa na inayohitaji mazoezi.

Wasanii waliosonga mbele  katika safari hiyo ni pamoja na MwanaFA, Shetta, AT na Amini. Wakati kwa upande wa wasanii wa filamu walioendelea ni Richie Richie, Ebitoke, Maya, Davina, Mariam Ismail, Dude na Husna Sagenti.