Dk Bashiru: Tanzania si nchi ya matajiri

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema nchi hiyo si ya matajiri, ni ya Watanzania wote

Dar es salaam.  Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema nchi hiyo si ya matajiri, ni ya Watanzania wote.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne  Agosti 27, 2019 katika uzinduzi wa shina la Wakereketwa  linaloundwa na madereva, makondakta na wajasiriamali wa eneo la Mbezi stand mtaa  wa Yusuph jijini Dar es Salaam.

Mtaa huo upo jimbo la Kibamba manispaa ya Ubungo ambalo mbunge wake ni John Mnyika wa Chadema.

"Nchi hii si ya matajiri, matajiri wanaweza kujitetea wenyewe, tunataka mashina haya yafanye kazi ya kutetea haki za wanyonge," amesema Bashiru.

Amebainisha kuwa kutokana na mapenzi ya Rais wa Tanzania,  John Magufuli kwa wananchi wanyonge, ameshatekeleza zaidi ya asilimia 90 ya ahadi za chama hicho alizozitoa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Amesema Serikali inashughulikia changamoto mbalimbali zinazogusa mahitaji ya Watanzania wanyonge, kuomba wakazi wa Ubungo kutomwangusha kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Dk Bashiru ameanza ziara katika wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Ubungo na Kibamba yaliyo chini ya Chadema.

Katika ziara hiyo anatembelea miradi mbalimbali, uzinduzi wa mashina ya chama hicho tawala na kufuatilia uhai wa chama  ikiwa ni miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.