Dk Bashiru ataka wana CCM kuwaheshimu wapinzani

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally leo Jumamosi amezindua mkakati wa kukomaza demokrasia kwenye mashina ulioandaliwa na CCM mkoa wa Dodoma.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewataka wanachama wa CCM kutobeza na badala yake kuheshimu alama za vyama vyote vya siasa nchini kwa sababu vimesajiliwa kisheria.

Dk Bashiru amesema hayo leo Jumamosi Machi 23, 2019, wakati akizindua mkakati wa kukomaza demokrasia kwenye mashina ulioandaliwa na CCM mkoa wa Dodoma.

Amewataka kutochoma wala kubeza alama za vyama hivyo na kwamba hivi karibuni kuna wafuasi wamechoma bendera na kupaka rangi ya chama chao ofisi za chama kingine.

"Ni kosa kuparamia na kupaka rangi ofisi za vyama hivyo. CCM tusifanye hivyo ni kosa kisheria. CCM tusifanye holela na uhuni huo katika siasa," amesema.

Ametaka wanachama wa CCM kuwa mfano bora na kwamba Serikali ina wajibu wa kulinda vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria.