Dk Bashiru awanyooshea kidole wabunge, wawakilishi

Muktasari:

Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania cha CCM, Dk Bashiru Ally ameanza ziara ya kukijenga chama hicho visiwani Zanzibar ambapo amewaonya wabunge na wawakilishi wa CCM wasiofanya kazi za wananchi wajiandae kuachia wengine.

Unguja. Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania cha CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho hakitawavumilia wabunge na wawakilishi wasiokua tayari kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi wajiandae kupoteza nafasi hizo.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 29, 2019 kisiwani Unguja, Zanzibar akiwa katika siku ya kwanza kati ya kumi ya ziara yake ya siku tisa kisiwani Zanzibar.

Amesema suala la wabunge na wawakilishi kushindwa kufanya kazi pamoja halikubaliki na kwamba chama hicho hakitawavumilia.

Dk Bashiru amesema mashirikiano kwa wabunge na wawakilishi sio suala la hiari kwenye chama hicho badala yake ni jambo la lazima na wasiokua tayari wakae pembeni kupisha wengine.

“Mwakilishi na mbunge wote ni zao la CCM lazima wakubali kufuata matakwa ya chama chao ni siyo kufuata uamuzi wao,” amesema Dk Bashiru

Pamoja na hayo amesema iwapo wabunge hao watashindwa kufanya kazi kwa pamoja wajijue kuwa wamepoteza sifa na chama hakitawapa tena nafasi hio.