Dk Ndugulile ataka asasi kuwasaidia wanawake vijijini kumiliki ardhi

Muktasari:

Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk Faustine Ndugulile amezitaka  asasi za kiraia kuwasaidia wanawake wa vijiji kwa maelezo kuwa wanakumbana na changamoto lukuki zinazowazuia kumiliki ardhi.


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk Faustine Ndugulile amezitaka  asasi za kiraia kuwasaidia wanawake wa vijiji kwa maelezo kuwa wanakumbana na changamoto lukuki zinazowazuia kumiliki ardhi.

Amesema licha ya sheria kutoa uwiano sawa kwa jinsia zote kumiliki ardhi bado wanakutana na vikwazo kupata umiliki wa rasilimali hiyo.

Dk Ndugulile ametoa kauli hiyo leo Novemba 21, 2019 wakati akizindua kampeni ya ‘Linda ardhi ya mwanamke’ inayolenga kuhamisha wanawake kumiliki ardhi.

“Tunafahamu bado kuna changamoto nyingi zinazomzuia mwanamke kumiliki  rasilimali ardhi na Serikali tunaendelea kuzifanyia kazi kuzimaliza.”

“Niziase asasi na mashirika yanayoshiriki kwenye kampeni hii yatawanyike nchi nzima kwa kuwa tatizo la wanawake kunyimwa haki ya kumiliki ardhi ni kubwa,” amesema naibu waziri huyo.

Mwenyekiti wa kamati inayoratibu kampeni hiyo,  Tike Mwambilikile amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutekeleza kampeni hiyo ya kimataifa inayoendeshwa na shirika la Landesa.

Amesema kampeni hiyo ya miaka 12 itaanza kwa utangulizi wa miaka mitatu ikiwa na malengo manne,  mojawapo ni kuondoa mila na desturi kandamizi zinazowakwamisha wanawake kumiliki ardhi.

Nyingine ni kuongeza wanawake kwenye ngazi za maamuzi ikiwemo mabaraza ya ardhi, kuwawezesha wanawake kutumia ardhi kwa manufaa ya kiuchumi na kulinda haki za mwanamke katika maeneo ya uwekezaji kwenye ardhi.

Awali, katibu mkuu wa wizara ya mifugo na uvuvi,  Profesa Elisante Ole Gabriel amewaasa wanaume kujifunza utamaduni wa kuandaa mgawanyo wa mali ili kuepusha migogoro.

“Ukiandika mapema na kuzigawa mali ikiwemo ardhi kwa mgawanyo sawa kwa watoto na mke itawafanya wawe na furaha na utaondoa uwezekano wa kutokea migogoro siku ukiwa haupo,” amesema.