Dk Ndugulile awazungumzia wagonjwa 53 waliolazwa Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile akizungumza katika kongamano kuhusu Haki za Mtoto linalofanyika jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

Wagonjwa 53 wa kata ya Mtumba jijini Dodoma wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya jiji hilo wakidaiwa kula chakula chenye sumu. Naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile ametoa tahadhari kwa jamii ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewataka wananchi nchini humo kuzingatia kanuni za afya hasa katika mikusanyiko ya watu kama misiba au sherehe.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Desemba 16, 2019 jijini Dar es Salaam na Naibu waziri wa Afya wa Tanzania, Dk Faustine Ndugulile wakati akizungumzia ugonjwa wa mlipuko uliotokea kata ya Mtumba jijini Dodoma.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea magonjwa ya kuhara kama ambavyo imetokea Mtumba.

Amesema wananchi na serikali za mitaa wanapaswa kuhakikisha uwepo wa maji safi na salama, choo na utumiaji wa vyakula ambavyo havijapoa.

Dk Ndugulile amesema tangu kutokea ugonjwa huo Desemba 14, 2019 hadi sasa kuna wagonjwa 53 kati yao wanawake 41, wanaume 12 na watoto watano.

“Wagonjwa wote walifikishwa hospitali wanaendelea vizuri, tunaendelea kufanya uchunguzi kwa kuchukua sampuli mbalimbali za wagonjwa na mabaki ya vyakula,” amesema

Dk Ndugulile amekanusha kuwepo kwa ugonjwa wa mlipuko katika mkoa wa Dar es Salaam kama inavyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Hakuna mlipuko wa ugonjwa wowote ndani ya Dar es Salaam, mifumo yetu ya ufuatiliaji ni imara. Tutaendelea kufuatilia kama kuna ugonjwa wowote na kujua chanzo chake ni nini.”

“Niwaombe watu watakaoona dalili zozote zisizo za kawaida kwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi. Jamii itoe taarifa kwa matukio ambayo sio ya kawaida ili hatua ziweze kuchukuliwa,” amesema Dk Ndugulile.