Dovutwa avuliwa uenyekiti UPDP

Muktasari:

Chama cha United People's Democratic Party (UPDP) nchini Tanzania kimemvua uenyekiti wa chama hicho, Fahmi Dovutwa baada ya kumtuhumu kufanya makosa yakiwamo ya chama hicho kutokushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019.

Unguja. Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha United People's Democratic Party (UPDP) imemvua uenyekiti Fahmi Dovutwa baada ya kubainika kufanya kosa la kukisemea chama hicho kinyume na katiba.

Uamuzi huo ulitangazwa jana Jumapili Desemba 2, 2019 Mjini Unguja, Zanzibar na Kaimu Mwenyekiti wa UPDP Taifa, Abdalla Mohammed Khamis akisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao hicho kujadili kwa kina makosa alioyafanya Dovutwa.

Alisema kosa kuu lililopelekea kuvuliwa kwa wadhifa wake ni kukisema chama hicho kuwa hakitoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa uchaguzi uliofanyika Novemba 24, 2019 Tanzania Bara kitendo ambacho alikifanya bila kuagizwa wala kupata ridhaa ya uongozi wa chama hicho.

"Alichokifanya Fahmi ni kukiuka katiba ya chama chake kwani hakupaswa kabisa kukisemea, uhalali wa kushirikiana au kutoshiriki uchaguzi huo na tunafanya hivi ili iwe ni funzo kwa viongozi wengine waliomo ndani ya chama na wanaokuja," alisema Kaimu mwenyekiti huyo.

Alisema suala la chama hicho kutoingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa imekiathiri kwani utekelezaji wa agizo alilotoa Dovutwa limesababisha chama kukosa  wenyeviti  wa serikali hizo ambao wataweza kuwakilisha chama.

Khamis alisema Dovutwa anaweza kukata rufaa endapo atahisi amevunjiwa haki yake kisheria na kikatiba na kwa sasa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida.

Pia, alisema kikao hicho kilimteua Twalibu Ibrahim  Kadege kuwa naibu  Katibu mkuu, ambapo kabla ya uteuzi nafasi hiyo ilikuwa wazi.

Mwananchi limemtafuta Dovutwa amesema atafutwe baadaye kwani yuko safarini kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam.

Itakumbukwa, UPDP ilikuwa miongoni mwa vyama sita vilivyosusia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019.

Vyama vingine ni; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, Chaumma na ACT-Wazalendo.