Exicab kuanza kutoa huduma ya teksi, magari ya mizigo Tanzania

Sunday September 15 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Huduma za uhakika za usafiri zimetajwa kuwa mojawapo ya kichocheo muhimu katika sekta ya utalii nchini Tanzania, hivyo wanaofanya kazi hizo wanapaswa kufanya kwa ufanisi na uaminifu mkubwa.

Hayo yameelezwa jana Jumamosi Septemba 14, 2019  na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Thomas Mihayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa app ya usafiri wa taksi inayofahamika kama Exicab iliyobuniwa na vijana wa Kitanzania.

Alisema sekta ya usafirishaji ni nguzo muhimu kwenye utalii hivyo uwepo uhakika wa huduma hiyo unahitajika kwa kiasi kikubwa katika kuwahudumia watalii.

“Watalii wanahitaji usafiri salama na wanaanza kuangalia mazingira kuanzia anavyoshuka uwanja wa ndege, usafiri unaombeba na mambo mengine. Hivyo vyote ndivyo vinaweza kumfanya siku nyingine arudi tena,”

“Kukiwa na usafiri wa kueleweka hata mtalii anakuwa na uhakika katika mizunguko yake bila hofu ya kuibiwa au kuvamiwa, ukarimu unahitajika mno kwenye kazi hii,” amesema

Ofisa mkuu wa operesheni wa Exicab, Norman Karamage ameeleza kuwa app hiyo imesajiliwa kwa kufanya kazi katika mikoa ya yote ya Tanzania lakini wataanza Dar es Salaam. Karamage alieleza kuwa hadi sasa zaidi ya madereva 300 wamejisajili wakiwemo wanawake 20.

Advertisement

“App yetu ipo katika muundo ambao inakupa nafasi ya kuchagua aina ya gari unalotaka na dereva, kama unataka dereva  mwanamke utachagua. Pia unaweza kuchagua gari lenye kiti cha mtoto,”

Alisema katika kuleta mapinduzi Exicab pia itakuwa na huduma ya magari ya mizigo hata ya kwenda mikoani.

Advertisement