Fatma Karume: Natafakari kuingia kwenye siasa

Sunday September 22 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakili nchini Tanzania, Fatma Karume amesema anatafakari kuingia kwenye siasa ili kuendeleza mapambano ya kupigania mabadiliko katika Taifa hilo ikiwa atazuiliwa kuendesha harakati hizo kupitia Mahakama.

Fatma ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 22, 2019 alipokuwa akijibu swali la Mwananchi lililotaka kujua uvumi kwamba huenda akajiunga na chama cha siasa baada ya kusimamishwa uwakili na Mahakama nchini humo.

Ijumaa iliyopita ya Septemba 20, 2019 mbele ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, Eliezer Feleshi alitoa uamuzi huo kwa madai katika wasilisho lake kwenye kesi ya Ado Shaibu ya kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Aderladus Kilangi, aliishambulia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Mpaka sasa hivi natafakari lakini nataka mabadiliko, hilo I will never give up on (sitalikatia tamaa). Hatuwezi kuishi kwenye nchi iliyokuwa na dhuluma kiasi hiki,” amesema Fatma katika mahojiano hayo.

Amesema kuna njia nyingi ya kutafuta mabadiliko mbali na Mahakama, miongoni mwa njia hiyo ni siasa. Amesisitiza kwamba anapenda kuona wananchi wanaheshimiwa, demokrasia inaheshimiwa na viongozi wanawajibika.

“Nataka kuona Mahakama inakuwa huru, nataka kuona watu wakienda mahakamani waheshimiwe, wapate haki zao, pengine ni mambo mengi ya kuomba, sijui,” amesema Fatma mtoto wa Rais wa zamani wa Zanzibar, Abeid Aman Karume huku akisisitiza kwamba huu ndiyo mwanzo kwake na siyo mwisho.

Advertisement

Katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, Fatma alisema pengine Mungu hapendi yeye kuendelea kuwa wakili na kwamba huenda siasa ndiyo eneo bora litakalomfaa zaidi.

Advertisement