Fisi avamia mjini Serengeti azua taharuki

Serengeti. Fisi ameibua taharuki kubwa kwa wakazi wa mtaa wa NHC Mugumu mjini wilayani hapa baada ya kuonekana akiranda mtaani na watu kuanza kumfukuza.
Tukio hilo limetokea leo Jumapili Machi 29 ambapo WAKATI akishambuliwa alikimbilia kwa balozi wa nyumba kumi Ismael Hassan na kuingia eneo walikohifadhi viti, hata hivyo  wananchi walifanikiwa kumtoa.
"Mimi nilikuwa sokoni ghafla nikapigiwa simu kuwa fisi ameingia nyumbani ambapo amemkuta mpangaji wangu  ambaye alikuwa jikoni, awali alidhani mbwa lakini ukubwa wake ukamstua akakimbia na kumwachia jiko," amesema balozi.
Hata hivyo, baada ya wananchi kumtoa akakimbia ghafla akaingia duka la Manginari Makuru na kuvunja kioo na kuzama ndani kwenye mifuko ya mchele.
"Mimi nilikuwa nimefuatilia kwa balozi wakati anatoka ndani kila mmoja alitawanyika, dukani niliacha mke wangu naye akawa ametoka, ndipo fisi akaingia ndani na kuvunja kioo cha kabati na kuingia ndani, watu wamejitahidi hadi kumtoa," amesema Makuru.
Hata hivyo wamefanikiwa kumtoa na kumshambulia kwa Mawe na kuokolewa na polisi na askari wa wanyamapori .
Ofisa wanyamapori wilayani hapa, John Lendoyani amesema kwa kuwa alikuwa hajafa wanaangalia hali yake  na wanaweza kumpeleka porini.