Fursa za mapinduzi mapya ya kiteknolojia zaanikwa

Aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu

Muktasari:

Tanzania imeonyesha utayari wa kukabiliana na awamu ya nne ya mapinduzi ya viwanda, huku wasomi wakibainisha fursa zake tele

 

Dar es Salaam. Tanzania imeonyesha utayari wa kukabiliana na awamu ya nne ya mapinduzi ya viwanda, huku wasomi wakibainisha fursa zake tele.

Katika awamu hiyo, uzalishaji wa bidhaa na utoaji huduma utafanywa zaidi na mifumo ya kiteknolojia kama roboti na mingineyo, na hivyo kuweka hatarini matumizi ya nguvu za mikono.

Hayo yalibainishwa jana wakati wa warsha iliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi ya Sahara Sparks, ubalozi wa Uswisi na kampuni ya Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA) ili kukutanisha wadau kujadili mapinduzi hayo.

Aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu alisema katika warsha hiyo kuwa mapinduzi ya kidigitali ni muhimu kwa kuwa yatafanikisha njia mpya za uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.

Profesa Ndulu, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa mshauri wa rais wa Afrika Kusini katika masuala ya uchumi, alisema teknolojia hivi sasa itatoa njia za kuongeza mavuno katika kilimo na utafutani wa masoko.

Alisema mapinduzi hayo yatachangia kuongeza uzalishaji na mtandao kama wa 5G, utakaorahisisha utoaji wa huduma na fursa za uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.

“Hadithi za sasa juu ya mapinduzi ya viwanda ni upotoshaji hasa katika nchi zinazoendelea, wanayaangalia zaidi katika kupotea kwa ajira katika uzalishaji,” alisema.

Lakini Balozi Ami Mpungwe ambaye ni mfanyabiashara, alisema mapinduzi hayo yanahitaji kujipanga katika sera na utamaduni, la sivyo ni vigumu kufanikisha.

“Tuna kila kitu cha kutufanya kufikia mapinduzi hayo, lakini tunakosa sera, mikakati na utamaduni ambao utatusaidia kuendana na teknolojia hiyo na mchakato wake,” alisema.

Hatua iliyofikiwa sasa, ilifafanuliwa na Dk Amos Nungu, mkurugenzi mkuu Costech.

“Tanzania inaenenda vizuri na sasa inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara. Ukitulinganisha na nchi nyingine za Afrika, utagundua kuwa wote tupo katika boti moja,” alisema Dk Nungu.

Mapema, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alisema: “Hii ni nyanja mpya katika maendeleo ya binadamu ambayo inatarajiwa kubadilisha namna ya kuishi na kufanya biashara.”

Alitoa wito kwa wadau wote “kutazama mapinduzi hayo na kujiuliza ni kwa kiasi gani wamejiandaa kunufaika nayo”.

Kaimu balozi wa Uswisi nchini, Leo Nascher aliungama na Ndalichako kusisitiza umuhimu wa wadau kuelewa namna ambavyo mapinduzi yanaweza kusaidia ubunifun unaotoa suluhisho kwa jamii.

Ni wakati sahihi sasa wa kujiuliza ni kwa namna gani mabadiliko yako yatagusa watu wa vijijini na mjini. Athari za mabadiliko haya zinaweza kuwa hasi au chanya, kujua na kuelewa jambo hilo ni muhimu sana,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliongeza kuwa mabadiliko katika teknolojia yanajiri kwa kasi ambayo haikutarajiwa na huenda kasi ikawa kubwa zaidi siku zinavyozidi kwenda.