Gambo aibua mjadala kibano cha watoa taarifa

Dar es Salaam. Agizo la kuwakamata watu waliopiga picha kuonyesha uharibifu wa barabara katika kreta ya Ngorongoro, limeibua suala jipya la kisheria kuhusu haki na wajibu wa watoa taarifa kwa nia njema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alitoa agizo wiki iliyopita baada ya picha zinazoonyesha uharibifu wa barabara za kreta hiyo uliosababishwa na mvua, kusambaa mitandaoni.

Gambo anaona kitendo hicho kililenga kuchafua utalii, lakini wanaomkosoa wanasema aliyepiga picha alikuwa na nia njema ya kuonyesha uharibifu ili mamlaka zichukue hatua, wakirejea sheria iliyotungwa na Bunge mwaka 2015 ya Kuwalinda Watoa Taarifa (Whistleblower and Witness Protection Act 2015).

Wanasheria wamesema sheria hiyo inawalinda pia waliotoa taarifa za ubovu wa barabara za Ngorongoro na masuala mengine ambayo mhusika anataka yarekebishwe.

Vifungu namba 10 na 11 vya sheria hiyo vinaeleza jinsi ambavyo mtoa taarifa anavyotakiwa kulindwa na kutotishiwa maisha, ama kutofukuzwa au kusimamishwa kazi au kupokea vitisho vya aina yoyote ile.

Vifungu 16 na 17 vya sheria hiyo vinatoa mwongozo kwa taasisi ambazo taarifa zao zimetolewa na mtoa taarifa, kuhakikisha zinachukua hatua za kushughulikia matatizo yao.

Gambo asema uhujumu uchumi

Lakini Gambo, ambaye alitembelea barabara iliyoharibika, aliliagiza Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuwasaka wahusika, akisema uharibifu wa miundombinu unatokana na mvua zinazoendelea na kwamba tatizo hilo haliko Tanzania pekee bali duniani kote.

Hivyo, alisema wanaosambaza picha hizo wana nia ya kuchafua taswira ya nchi ili kuzuia watalii kuja kutembelea vivutio, jambo ambalo alisema ni uhujumu uchumi. Alisema watu hao wangeweza kufikisha kilio chao katika mamlaka husika badala ya kuzisambaza katika mitandao ya kijamii.

Polisi inaendelea na msako huo na hadi jana hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa.

Msimamo huo wa Gambo umekosolewa na wanasheria waliozungumza na Mwananchi wakisema waliosambaza picha hizo hawakufanya kosa lolote, bali walitoa taarifa kwa mamlaka husika na zikachukua hatua na kwamba kama kuna kosa lililofanyika basi mamlaka husika ndiyo yenye dhamana.

“Sheria haimruhusu (mkuu wa mkoa) kutoa amri ya kukamata watu wanaosambaza taarifa za matatizo ya miundombinu ya Ngorongoro,” alisema mkurugenzi wa Kituo cha Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Onesmo Olengurumwa.

Olengurumwa alisema watoa taarifa wana uhuru wa kufanya hivyo kwa kuwa wanalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Katiba inawalinda watoa taarifa hawa kwa kuwa inawapa haki ya kutafuta na kutoa habari ili mradi zisiwe za uongo wala uchochezi. Hakuna kosa kwa mtu kutoa taarifa kama kuna tatizo katika eneo lake,” alisema.

“Pia watu hawa hawapaswi kusumbuliwa kwa kuwa wanalindwa na sheria ile ya kulinda watoa taarifa na ile ya upashanaji habari.”

Olengurumwa alisema ikitokea watu wakakamatwa kwa amri ya Gambo, basi wao kama watetezi, wapo tayari kuwatetea kama walivyofanya kwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliokamatwa baada ya kutoa taarifa za matatizo tofauti vyuoni kwao.

Watoa taarifa waliobanwa

Ikiwa waliosambaza picha hizo watakamatwa, wataingia katika orodha ya watu waliotoa taarifa kwa lengo la kutaka matatizo yashughulikiwe, wakaingia matatani na mamlaka.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Kumbusho Dawson alikamatwa na polisi Desemba 4, 2017 kwa kusambaza picha zinazoonyesha nyufa katika majengo ya hosteli ya chuo hicho.

Katika tukio jingine, viongozi watano wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) walisimamishwa kwa kosa la kuitisha mkusanyiko na kutishia kuandamana kama wanafunzi wenzao wasingepewa mkopo.

Viongozi hao waliosimamishwa Desemba 19, mwaka jana ni pamoja na Rais wa Daruso, Hamisi Musa Maulid, Waziri wa Mikopo, Malekela Joseph Brighton, Waziri wa Habari, Judith Mariki Godson, mwenyekiti wa Bunge, Ititi Kassim Mussa na Milanga Hussein Hassan, ambaye ni mwenyekiti wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi na hadi sasa hawajarejeshwa chuoni.

Pia, mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea Shahada ya Sayansi katika Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Mugaya Tungu alikamatwa Januari 21, 2020, akiwa ndani ya bwenini kwa kusambaza picha za matatizo ya maji chuoni hapo.

Ngorongoro ina sheria yake

Kuhusu sakata la Ngorongoro, wakili wa kujitegemea, Francis Stolla alisema hifadhi hiyo huratibiwa na sheria na kanuni za mamlaka husika.

Alisema kama mtu akipiga picha bila kibali, hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria za mamlaka hiyo na ndiyo yenye wajibu wa kuchukua hatua.

Alisema sheria ya mamlaka hiyo kwa makosa yanayohusiana na shughuli za hifadhi, haiwezi kuingiliwa na sheria nyingine kama Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai wala ya uhujumu uchumi.

“RC (Mkuu wa mkoa) humwakilisha Rais na anafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa. Hivyo mle ndani ya hifadhi hana mamlaka kwa kosa linalohusu shughuli za hifadhi,” alisema wakili Stolla.

Wakili mwingine, Fulgence Massawe alisema hifadhi ni eneo la kibiashara na kwamba waliopiga picha hizo walitoa tu taarifa za hali hiyo.

“Hao ni whistleblowers (watoa taarifa) ambao wamefichua uharibifu ili hatua zichukuliwe na mamlaka husika na hulindwa na Sheria ya Ulinzi dhidi ya Mtoa Taarifa na Shahidi,” alisema wakili Massawe.

Alisema sheria hiyo inatoa ulinzi kwa watoa taarifa za uhalifu na mashahidi, kwamba hawatatajwa kutokana na kutekeleza wajibu huo.

Hoja za wakili Massawe zinalingana na za wakili mwingine wa kujitegemea, Juma Nassoro ambaye naye alisema agizo la Gambo amelitoa pengine kutokana na kutojua sheria.

Alisema upo umuhimu wa viongozi kuelimishwa masuala ya sheria kama ya uhujumu uchumi ili wawe na ufahamu.

“Kwa agizo hilo, ni dhahiri lipo tatizo la uelewa wa madhumuni na mipaka ya sheria hiyo,” alisema wakili huyo.

“Kuonyesha uharibifu wa kitu hakuwezi kuwa kosa la uhujumu uchumi kwa kuwa halipo katika makosa ya uhujumu uchumi wala la jinai.”