ELIMU BILA MALIPO: Gharama za mahitaji sababu ya watoto kutojiunga sekondari

Mikoani. Wakati waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wakiendelea na masomo, imeelezwa kuwa gharama za mahitaji ya mwanafunzi ni moja ya sababu kubwa zilizochangia maelfu ya watoto kushindwa kuripoti shuleni.

Hadi Alhamisi, ikiwa ni siku 16 tangu waripoti katika shule walizoteuliwa, ni asilimia 55 tu ya wanafunzi waliokuwa wameripoti, lakini kaimu kamishna wa elimu, Dk Lyabwene Mtahaba alisema mahudhurio ni mzuri kwa kuwa muda wa kuripoti ni siku 90.

Mwananchi iliibua habari hiyo baada ya kuongea na maofisa elimu katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Mara na Geita.

Idadi ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari iliongezeka mwaka huu, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yanayoonyesha asilimia 81.50 ya wanafunzi 933,369 waliofanya mtihani mwaka 2019 walifaulu.

Serikali imeamua kutoa elimu bure kuanzia ya msingi hadi sekondari, lakini idadi ya wanafunzi walioshindwa kuripoti shuleni hadi sasa imekuwa kubwa licha ya ukweli kwamba baadhi watajiunga na shule binafsi ambazo wazazi wao wanaamini zinatoa elimu bora zaidi.

Wananchi waliozungumza na gazeti hili wameeleza kuwa mahitaji ya shuleni kama sare, vitabu, chakula, madaftari na vifaa vingine maalum kwa ajili ya baadhi ya shule umekuwa mzigo.

Baadhi ya shule zinataka wanafunzi waende na takriban madaftari 20 makubwa yanayouzwa kati ya Sh2,500 na Sh3,000.

Wazazi wengine wamesema suala la kupeleka watoto wao shule za sekondari halikutegemewa wala halikuwa kipaumbele kwao na hivyo hawakuandaa fedha kwa ajili hiyo.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dodoma walisema hali ngumu ya maisha ndiyo iliyowasababishia kutowapeleka watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza mpaka sasa.

Josephine Eliya, ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo katika jiji la Dodoma, alisema amekuwa akihangaika kwa muda mrefu sasa ili ampatie mwanaye mahitaji muhimu ili aende shuleni, lakini imeshindikana kutokana na hali kuwa ngumu.

Alisema mwanaye alipangwa kwenda Shule ya Sekondari ya Sechelela lakini kwa muda wote huo ameshindwa kumpeleka kutokana na kushindwa kukamilisha mahitaji muhimu yanayotakiwa shuleni.

Lakini ofisa elimu ya Sekondari Dodoma, Martin Nkwabi alisema ikifika Februari watafanya msako wa watoto wote ambao wamefaulu na hawajajiunga na kidato cha kwanza na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Jiji la Dodoma lilifaulisha wanafunzi 8,886 lakini walioripoti mpaka Januari si wote.

Mkazi wa Matare, Gabriel Mwita alisema mtoto wake amepangwa Shule ya Sekondari ya Robanda na mahitaji yake ni zaidi ya Sh800,000, gharama ambazo wazazi wengi wanashindwa kuzimudu.

“Gharama ni kubwa sana, unatakiwa ununue kilo 72 za mahindi, maharage kilo 30, mchele kilo 25, sukari kilo 5, majembe, ndoo, nguo za shule, sare na mambo mengi,” alisema.

“Ukipiga hesabu inafikia Sh800,000 hiyo ni shule ya kata kwa kuwa kuna bweni, mazingira kama hayo wazazi tunashindwa.”

Mkoani Shinyanga, mkazi wa Majengo anayeitwa Paul Sangija na ambaye mtoto wake amechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Ndala, alisema sababu bado anatafuta fedha za kumshonea sare na kununua madaftari kutokana na kipato duni.

“Kipato changu kwa siku ni Sh2,000, kutokana na kazi yangu ya kufanya usafi kupalilia majani na kufyeka nyasi na wakati mwingine naweza nisipate kazi,” alisema.

“Fedha hii ndiyo nategemea familia ipate chakula. Sasa nikusanye kidogokidogo hadi kupata ya kununua uniform (sare) Sh25,000 shati na suruali.”

Naye Annastazia Jackson mkazi wa Ngokolo, Shinyanga alisema changamoto kubwa aliyonayo ni kukosa fedha za kumnunulia sare.

Lakini Evalist Kabalo anayeishi kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga, alisema wazazi wengi wana kipato cha chini hivyo wanafanikiwa kupate hela kidogo ya chakula.

“Licha ya Serikali kuondoa ada, bado mahitaji yanawasumbua, natakiwa kumnunulia madaftari makubwa moja linauzwa Sh3,000, anaihitaji sare za shule, hivyo natakiwa kama Sh50,000 hivi ili mtoto aende shule,” alisema.

Mwananchi ilimtafuta Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Technolojia, William Ole Nasha ambaye alisema ni makosa kwa wazazi kutowapeleka shule wanafunzi.

Ole Nasha alisema wazazi hawana sababu ya kutopeleka shule watoto kwa kuwa serikali inatoa elimu bure.

“Sheria zipo wazi, elimu ya sekondari hivi sasa ni lazima kwa watoto, sasa kama mtoto amefaulu halafu mzazi hataki kumpeleka shule akibainika, atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema

Kuhusu michango, Ole Nasha alisema ni marufuku shule kukusanya fedha bila kupata kibali cha Serikali.

“Serikali ilifuta michango yote ambayo ilikuwa haina tija, sasa kama kuna walimu wanachukua fedha bila kufuata taratibu tupeni taarifa,” alisema.

Ole Nasha aliwataka wazazi kupeleka watoto shule na kwamba michango yote shuleni ni lazima ipate kibali cha wakurugenzi wa halmashauri.

Tatizo la kiuchumi

Mbali na mahitaji ya shule kugharimu fedha nyingi, baadhi ya wazazi wanaona kipato hafifu ndio sababu kubwa.

Mmoja wa wazazi wa Kitongoji cha Katuma mkoani Rukwa, John Samweli, ambaye mtoto wake amefaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Kasanga wilayani Kalambo alidai baada ya matokeo kutoka na kuonyesha mtoto wake Peter Samweli amefaulu, alianza kutafuta fedha za kununua mahitaji mbalimbali lakini hakufanikiwa.

“Unajua hali ya maisha imebadilika sana,” alisema.

“Sasa nimejaribu kuuza mazao niliyokuwa nimehifadhi ndani lakini sikufanikiwa kupata mteja. Sasa nimeshusha bei ya mahindi gunia kutoka Sh80,000 hadi Sh65,000 labda naweza kupata mteja ili nipate fedha za kununua mahitaji ya mtoto wangu.”

Naye, Maria Simkonda, mkazi wa kijiji cha Ntatumbila wilayani Nkasi, ambaye mtoto wake Dayana Moses alifaulu kwenda Shule ya Sekondari Kirando, alidai kuwa upatikanaji wa fedha ndio tatizo kwake, na ndio maana mtoto wake hajaanza kidato cha kwanza.

Katika mikoa ya Lindi na Mtwara, tatizo hilo la watoto kutojiunga na sekondari hadi sasa limehusishwa na malipo ya korosho kuchelewa.

Mkazi wa Lindi, Rashid Hassan alisema wazazi wengi walioshindwa kuwapeleka watoto shuleni wanapoulizwa sababu wanasema ni ucheleweshwaji wa malipo ya fedha za msimu wa mwaka 2019/20.

“Wamepeleka mazao yao ghalani lakini baadhi ya wakulima hawajalipwa, wengi ambao bado hawajapeleka watoto wao shule sababu wanayotoa ni hiyo wengine ni matatizo kwenye vyama vya ushirika hesabu hazijakaa vizuri kwa hiyo bado hawajalipwa,” alisema Hassan.

Imeandikwa na Mussa Juma (Arusha) Joseph Lyimo (Manyara), Anthony Mayunga ,Twalad Salum (Serengeti), Stella Ibengwe, Suzy Butondo (Shinyanga) Robert Kakwesi, (Tabora) Rachel chibwete (Dodoma) Haika Kimaro (Mtwara) Lilian Lucas(Morogoro) na Mussa Mwangoka (Rukwa).