Giza la siku mbili Kagera lapeleka timu ya wataalamu wa Tanesco

Muktasari:

Maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera yako gizani kwa siku ya tatu baada ya kukosekana kwa huduma ya umeme. Maeneo mengi ya mkoa huo yameunganishwa na gridi ya Taifa ya Uganda.


Bukoba. Wakazi wa Mkoa wa Kagera wameendelea kukaa gizani baada ya kukosa huduma ya umeme.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 21, 2019, na Mwananchi kwa simu, Ofisa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji amesema chanzo cha tatizo hilo ni njia ya umeme inayolisha mkoa huo kutoka kwenye gridi ya Taifa ya Uganda kutoka.

“Maeneo mengi ya mkoa wa Kagera yanapata umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa ya Uganda, kuna tatizo limetokea eneo la Mutukula, Uganda, limesababisha njia inayolisha umeme Kagera kutoka, ndiyo maana umeme umekatika,” amesema Leila.

Hata hivyo, amesema tayari timu ya wataalamu wa Tanesco kutoka Kanda ya Ziwa na wa Wizara ya Nishati wameshaondoka nchini kuelekea Mutukula kwenda kubaini chanzo cha tatizo.

“Wataalamu wetu wameondoka jana wameenda kushughulikia tatizo hilo kwa kushirikiana na wenzao wa Uganda ambao bado hawajaeleza chanzo hasa ni nini. Hivyo tunasubiri kupata majibu kutoka kwao,” amesema Leila.

Habari kutoka Kagera zinasema kukatika huko kwa umeme kumeathiri pia shughuli za kijamii kama huduma ya maji ya bomba.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti akizungumzia tatizo hilo leo alipozungumza na Mwananchi, amesema tayari Waziri wa Nishati, Medard Kalemani naye ameelekea Uganda kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.

“Tatizo lipo upande wa Uganda, si hapa kwetu ndiyo maana Waziri ameenda huko,” amesema Gaguti.

Tangu kukatika kwa umeme juzi, maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera ukiwamo mji wa Bukoba yameathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na kukosa huduma muhimu.

Huduma hizo ni pamoja na maji ambayo yamekatika baada ya mitambo ya kusukuma maji ya Mamlaka ya Majisafi na taka  (Buwasa) kushindwa kufanya kazi.

Baadhi ya wananchi wameonekana wakiwa wamebeba ndoo na madumu wakifuata maji Ziwa Victoria na maeneo mengine yasiyo salama, hali inayotishia mlipuko wa maradhi.

Pia wale wanaomiliki simu za mkononi, wanapishana kwa wingi kwenye maeneo ya wafanyabiashara waliowasha jenereta ili kupata huduma ya kuzichaji.

Kwa mujibu wa Leila, taarifa za ufumbuzi wa tatizo hilo zitaendelea kutolewa na Tanesco kwa wananchi kila zipatikanapo.

“Tunaendelea kuwasiliana na timu iliyoenda Mutukula, kwa hiyo tutaendelea kutoa taarifa ya nini kinaendelea hatua kwa hatua,” amesema Leila.