HOJA ZA KARUGENDO: Tusisubiri miti, mawe yaulize maswali haya

Thursday March 19 2020

 

By Padri Privatus Karugendo

Nimeamua kuuliza maswali Nimeamua kuuliza maswali haya, maana lazima atokee mtu wa kuyauliza. Haiwezekani tukasubiri miti na mawe ndiyo yaje kuuliza maswali haya. haya, maana lazima atokee mtu wa kuyauliza. Haiwezekani tukasubiri miti na mawe ndiyo yaje kuuliza maswali haya.

Kila Mtanzania aliyesoma na anayeguswa na uhai wa Taifa, lazima ayaulize kwa sababu tunaelekea kujenga utamaduni wa kusema, “Yakitokea nitakuwa nimeondoka.” Huu ni utamaduni wa kuishi leo bila kufikiria maisha ya vizazi vijavyo, tunaitaka Tanzania ya leo bila kutilia maanani Tanzania ya kesho na keshokutwa. Tunaipiga kisogo historia ya Baba zetu waliopigana kufa na kupona ili tupate uhuru, tuishi kwa heshima kama binadamu wote na kurithisha uhuru huu na neema zote kwa vizazi vijavyo. Nimeamua kuuliza maswali haya kwa vile tumejenga utamaduni wa kuogopana na kuoneana aibu; tumejenga utamaduni wa kutanguliza vyama vya siasa badala ya kulitanguliza taifa letu.

Tumejenga utamaduni wa kuwatanguliza marafiki na ndugu zetu badala ya Taifa.

Tumejenga utamaduni wa kuwaona wale wote walio kwenye vyama vya upinzani kama wasaliti wa watu kutoka nje ya nchi.

Tumejenga utamaduni wa kuyakomboa majimbo yaliyo kwenye mikono ya wapinzani kana kwamba wao ni watu wa Burundi au Rwanda. Neno lenyewe “Kukomboa” linajieleza vizuri. Tumejenga utamaduni wa kuiweka pembeni Katiba yetu na kutenda kwa kuongozwa na ushabiki na mpenzi ya vyama vyetu vya siasa. Tunajenga utamaduni wa kuishi leo bila kufikiria kesho ya watoto wetu na wajukuu zetu.

Ni nani huyu anayeanzisha utamaduni huu. Lazima ajitokeze mtu wa kusema liwalo na liwe.

Advertisement

Lazima ajitokeze mtu wa kukemea na kuonya! Kuna rafiki yangu wa karibu ameniambia leo hii Tanzania hakuna wakusimama na kukemea. Wazee wetu Marais wastaafu wamekaa kimya! Wanasubiri kuondoka au? Ninauliza maswali haya nikijua baadhi ya wengine wataguswa, wataumia na kuchukia, nazingatia ukweli kwamba baadhi ni rafiki na ndugu zangu wa karibu; sipendi kabisa kuwasaliti, lakini kwa suala la kitaifa niko tayari kumsaliti baba, mama, kaka, dada na rafiki wa karibu. Nauliza maswali haya kwa kutambua kwamba Taifa letu limeanza kuyumba.

Tukianza kutoka kwenye misingi na kupoteza utamaduni wetu ni dalili mbaya kwa Tanzania ya kesho. Tumeshuhudia wabunge kina Halima Mdee na Ester Bulaya pamoja na wanawake wengine wakipigwa hadi kuumizwa pale Segerea. Huu ni utamaduni wa Mtanzania? Wabongo, watatukanana kwenye daladala hadi matusi ya nguoni, lakini ustaarabu wa “Mtanzania” hawapigani.

Kupigana ni hatua ya kuuvua ubinadamu! Je Tanzania tunaelekea huko? Ninauliza! Ni nani anaanzisha utamaduni mpya wa kuwapiga watu? Kwamba hatuwezi kuzungumza tukaelewana hadi tupigane, mpaka tuumizane? Tunaishiwa hoja? Tunaogopa majadiliano? Wakati dunia nzima inapigia kelele 50/50, tunaanzisha utamaduni wa kuwapiga wanawake?

Utamaduni wa kuwapiga viongozi ambao ni wawakilishi wa wananchi ni sawa na kuwapiga wananchi.

Tanzania tumejengewa utamaduni wa “Udugu” utamaduni wa kuheshimiana, sasa ni nani huyu anaanzisha utamaduni mpya ambao ni kinyume na Haki za Binadamu na kinyume na ustaarabu wa dunia hii. Ninauliza ili nipatiwe majibu.

Ninauliza, mbona kimya kimetawala kana kwamba hakuna chochote kilichotokea? Kuna kukanusha tu!

Nauliza tena, Muhimu ni chama cha siasa au Taifa? Tushughulikie nini kuendeleza vyama vya siasa au kuliendeleza taifa la Tanzania?

Wenye mawazo yanayofanana, mfano kwa suala wa ufisadi kwa nini wasiungane na kuwa na sauti moja hata kama wanatoka vyama tofauti?

Tunashuhudia kwamba baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani wana mawazo yanayofanana juu ya ufisadi.

Lakini saa ikiwadia, vyama vinakuwa na nguvu zaidi ya utaifa.

Hoja yangu ni kwamba tufumbue macho kwa jambo hili. Tuache kufanya mambo kwa ushabiki, bali tufanye kwa kuangalia maendeleo ya Tanzania ya leo na ya kesho. Na tutafanya hivyo kwa kukubali mawazo tofauti, sera tofauti na vyama tofauti, tukiwa na lengo la kulijenga taifa letu. Tanzania, ni yetu sote. Hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine!

Advertisement