Habinder Seth aandika barua kwa DPP kukiri makosa

Muktasari:

Habinder Seth anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa yake na kuomba msamaha.

Dar es Salaam. Habinder Seth anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa yake na kuomba msamaha.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Seth, mwenyekiti mtendaji wa PAP pamoja na James Rugemalira ambaye ni mkurugenzi wa VIP wanakabiliwa na mashtaka 12 wanayodaiwa kuyatenda jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi na kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 309bilioni.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama hiyo  Juni 19, 2017 na hadi sasa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Katika mahakama hiyo upande wa mashtaka uliombwa na upande wa utetezi kuwasaidia kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umechukua muda mrefu, kutaka ielezwe ni lini utakamilika.

Baada ya maelezo ya hayo, Wankyo Simon ameeleza kuwa  wamepokea barua ya Seth wanaifanyia kazi na majibu yatatolewa.

Kuhusu upelelezi wa kesi hiyo, Wankyo amesema bado haujakamilika na hawezi kuahidi utakamilika lini.

Baada ya kusikiliza pande zote Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 24, 2019.