Hatima ya Kinana, Makamba na Membe baada ya siku saba

Muktasari:

  • Leo Jumatano Februari 12, 2020  Mwenyekiti wa Chama tawala nchini Tanzania CCM, Rais John Magufuli ameongoza kikao cha kamati kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam na kujadili masuala mbalimbali ikiwamo la kuhojiwa kwa wanachama wake watatu, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba Bernard Membe wanaokabiliwa na tuhuma za kimaadili.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimetoa siku saba kwa

kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe na kuiwasilisha katika vikao husika.

Kinana na Makamba ambao ni makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho na Membe aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania walifika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula kuhojiwa juu ya tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 12, 2020 ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema wanachama hao tayari wamekwisha kuhojiwa na taarifa yao inasubiriwa.

Kinana, Makamba na Membe waliitwa mbele ya kamati ya maadili Desemba 13 mwaka 2019 baada ya sauti zao kuenea katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto, uendeshaji nchi na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu huo dhidi ya mtu anayewachafua.

Sauti hizo zilizoanza kusambaa mitandaoni baada ya waraka wa Kinana na Makamba kuutoa Julai 14 mwaka 2019 wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa wakiwadhalilisha na ambaye walimwelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Wakati Membe akihojiwa Februari 6, 2020 makao makuu ya CCM, White House jijini Dodoma, Makamba na Kinana wao waihojiwa na kamati hiyo Jumatatu iliyopita ya Februari 10, 2020.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika leo Jumatano Februari 12, 2020 kutoa taarifa ya maazimio ya  kikao cha kamati kuu kilichoongozwa na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, Polepole amesema pamoja na mambo mengine kimepokea taarifa za maandalizi ya mwelekeo wa sera za CCM kwa mwaka 2020 – 2030 na Ilani ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Kamati Kuu imepokea taarifa ya maendeleo ya uandishi wa waraka huu muhimu wa kisera na kujiridhisha na kazi nzuri ambayo imekwisha kufanyika mpaka ngazi ya rasimu.”

“Kamati kuu pia imepitia zoezi la uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kuagiza maoni ya wadau mbalimbali kujumuishwa na kuzingatia ratiba ya kukamilisha uandishi wake ili vikao vya chama vifanye uamuzi na kupitisha,” amesema Polepole

Polepole amesema kamati kuu imepokea maombi kujiunga na uanachama wa CCM kutoka kwa waziri mkuu wa zamani wa Tanzania, Fredreck Sumaye ambaye Jumatatu ya Februari 10, 2020 alitangaza kurejea katika chama hicho baada ya kukihama Agosti 22 mwaka 2015 na kujiunga na Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.