Hiki ndicho kilichojiri kesi ya Shamimu, mumewe

Muktasari:

Upelelezi katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida(45)na mkewe, Shamim Mwasha(41) bado haujakamilika.

Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha (41) bado haujakamilika.

Nsembo na Shamimu wakabiliwa na  shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin, kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbali na kutokukamilika kwa upelelezi huo, upande wa mashtaka amedai leo Jumatano Novemba 27, 2019  kuwa  bado unasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Wakili wa Serikali Wankyo Simon ameieleza mahakama hiyo wakati shauri hilo, lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Simon ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Simon.

Hakimu Mhina, baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6, 2019 itakapotajwa na washtakiwa  wamerudishwa rumande.

Hata hivyo, mshtakiwa Nsembo ameshamuandikia barua ya kukiri na kuomba msamaha, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania(DPP).

Kwa mujibu  wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, Jijini Dar Es Salaam.

Siki hiyo ya tukio, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gram 232.70, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Kwa mara  ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Mei 13, 2019.