Hospitali ya Bugando yaanza kutekeleza agizo la Magufuli

Muktasari:

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) jijini Mwanza kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki cha Afya na Sayansi (Cuhas) wameanza kufanya utafiti kubaini chanzo cha ugonjwa wa saratani katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) jijini Mwanza kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki cha Afya na Sayansi (Cuhas) wameanza kufanya utafiti kubaini chanzo cha ugonjwa wa saratani katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Uchunguzi huo unafanyika kutokana na wagonjwa wengi wa magonjwa yasiyoambukiza kudaiwa kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, jambo ambalo Rais wa Tanzania, John Magufuli Julai 15, 2019 aliiagiza  hospitali hiyo na wadau wengine kufanya uchunguzi.

Magonjwa mengine yanayofanyiwa utafiti ni moyo, kisukari, mgandamizo wa moyo, figo na uzito kupita kiasi.

Katika maelezo yake Magufuli alisema zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam wanatoka katika mikoa hiyo.

Mkurugenzi wa Bugando, Professa Abel Makubi amesema utafiti huo wa awali unalenga kubaini vyanzo na viashiria vya magonjwa hayo.

“Huu ni utafiti wa awali, Bugando kwa kushirikiana na Cuhas tumeamua kuanza kufanya utafiti huu kubainia viashiria. Utafanyika mikoa sita na wilaya 12 katika ngazi ya vijiji  kwa kuwafuata wananchi ili tuweze kuja na takwimu halisi za matatizo haya,” amesema Professa Makubi

Amesema katika utafiti huo utakaogharimu Sh60 milioni, unalenga kuwafikia wananchi 770 kujua viashiria vinavyoweza kuhusika na magonjwa hayo, uelewa wa watu kuhusu magonjwa hayo, pia uwezo wa vituo vya afya kwenye maeneo hayo.

“Tuna data zisizotosheleza  na wengi tunaowaona ni wale wanaokuja hospitalini lakini wapo wengi hawafiki, kwa sasa katika hospitali yetu kila siku tunaona wastani wa wagonjwa watano wa shinikizo la dawamu. Asilimia 25 hadi 30 ya wagonjwa waliopo wodini wana ugonjwa huo huku kwenye kliniki ya kila wiki wanaonwa wagonjwa 70,” amesema.

SOMA ZAIDI

amesema wagonjwa wa kiharusi kuna kesi mbili kwa wiki huku wagonjwa wanaosafishwa figo wakizidi 100.

Mhadhiri mwandamizi wa Cuhas,  Dk Anthony Kapesa amesema utafiti huo utahusisha madaktari bingwa 12 na watafiti wasaidizi zaidi ya 200. Kati ya madaktari hao wawili watakuwa wakiangalia ufanyaji kazi wa moyo.

Alizitaja wilaya zitakazopitiwa na utafiti huo na Mikoa zilizopo katika mabano kuwa ni Bunda, Serengeti (Mara); Bariadi, Busega (Simiyu); Geita, Chato (Geita); Muleba, Bukoba Vijijini (Kagera); Shinyanga, Kishapu (Shinyanga) na Sengerema, Misungwi (Mwanza).

Mkurugenzi wa utafiti wa Cuhas, Professa Domenica amesema, “Tumefanya  hivi ili tuwe na uhakika na uhalali wa takwimu badala kusema bila utafiti hivyo tunaomba wananchi wote watakaopitiwa na utafiti huu watupe ushirikiano wa kutosha kufanikisha shughuli hii.”