Hukumu kesi ya kina Mbowe yaanza kusomwa

Muktasari:

Hukumu ya kesi inayowakabili viongozi wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe imeanza kusomwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Machi 10, 2020 saa 7:00 mchana.

Dar es Salaam . Hukumu ya kesi inayowakabili viongozi wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe imeanza kusomwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Machi 10, 2020 saa 7:00 mchana.

Hukumu hiyo inasomwa na Hakimu Mkazi mkuu wa Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba huku ulinzi ukiwa umeimarishwa ndani, nje ya mahakama hiyo.

Hukumu hiyo inasomwa katika mahakamani ya wazi  namba moja. Idadi kubwa ya wananchi na wafuasi wa chama hicho wamezuiwa kuingia mahakamani, kutakiwa katika nje.

Katika kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kati ya Februari 1 na 16, 2018.

Viongozi mbalimbali wa Chadema wakiwemo wabunge na wenyeviti wa kanda  ni miongoni mwa waliojitokeza kusikiliza hukumu hiyo.

Wengine ni kutoka vyama vingine vya upinzani akiwemo mshauri mkuu wa ACT- Wazalendo,  Maalim Seif Sharif Hamad.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Esther Matiko (Tarime Mjini); Halima Mdee (Kawe); Ester Bulaya (Bunda) na John Heche (Tarime Vijijini).