Huyu ndio bilionea Ali Mufuruki

Muktasari:

  • Mwili wa mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki umezikwa jana Jumanne Desemba 10, 2019  katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam baada ya kuagwa katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), huku maelfu ya watu ndani na nje ya nchi wakiendelea kumlilia.

Dar es Salaam. Mwili wa mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki umezikwa jana Jumanne Desemba 10, 2019  katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam baada ya kuagwa katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), huku maelfu ya watu ndani na nje ya nchi wakiendelea kumlilia.

Maombolezo ya bilionea huyo nchini yanatokana na jinsi alivyogusa maisha ya wengi.

Mwili wa Mufuruki aliyefariki dunia alfajiri Desemba 8, 2019 uliwasili nchini juzi ukitokea Afrika Kusini na kuagwa jana.

Mufuruki alifariki dunia katika Hospitali ya Morningside iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini alikopata matibabu kwa siku moja akitokea Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa wiki moja akisumbuliwa na homa ya mapafu (nimonia).

Enzi za uhai wake, Mufuruki (61) aliongoza na kushiriki katika masuala tofauti kwenye bodi za mashirika ya umma na binafsi huku akianzisha kampuni zilizogusa maisha ya wananchi wengi.

Ukiacha ushauri alioutoa kwa menejimenti za kampuni na mashirika alikoteuliwa, alikuwa na kampuni zilizotoa huduma zinazotumiwa na wananchi wa kada zote.

Alikuwa mmiliki wa kampuni ya visimbuzi vya Zuku vinavyopatikana Tanzania, Uganda na Kenya.

Akimpa pole Saada, ambaye ni mjane wa marehemu, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Nation Media Group (NMG) ya Kenya, Wilfred Kiboro alisema Mufuruki alikuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wengi.

“Wengi tutamkumbuka mumeo kwa uwezo wake wa kuhoji, kutia moyo na alivyoamini katika ujasiriamali wa Kiafrika. Alikuwa mchapakazi aliyependa kuwasaidia wengine, alikuwa mjuzi wa masuala ya uongozi wa kampuni ambaye ni hazina si kwa Tanzania pekee bali Afrika nzima,” alisema Kiboro.

 

Enzi ya uhai wake, Mufuruki amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa NMG na mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Akitambua mchango wake katika utumishi ndani ya kampuni hizi mbili, Kiboro alisema: “kwa niaba ya bodi ya NMG tunaiombea familia na ndugu zake katika kipindi hiki kigumu.”

Mwingine aliyeguswa na msiba wa Mufuruki ni mwanamuziki maarufu wa Afrika Kusini, Yvonne Chakachaka ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika, “Novemba 7, mwezi mmoja tu uliopita nilikutana naye na akazungumza mambo mazuri kuhusu Afrika, alinitia moyo, alisema ni lazima tuifanye Afrika vile tunavyopenda, nilikuwa nasubiri utekelezaji wa maneno haya ya kaka yangu, lakini kifo hakieleweki, huwezi kujivunia, hii ni kama ndoto mbaya.’’

Licha ya huduma za mawasiliano kupitia runinga, Mufuruki aliwekeza kwenye teknolojia na kampuni yake ya Simbanet na taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha ilipata leseni itakayodumu kwa miaka 25 tangu Aprili 25, 2011.

Kupitia kampuni hiyo, Mufuruki anaziunganisha kampuni na baadhi ya makazi kwa intaneti ya uhakika.

Kupitia kampuni yake ya W-Stores Mufuruki ndiye mmiliki wa maduka yanayouza nguo za Woolworths yakiwa na matawi jijini Dar es Salaam na Arusha Tanzania na Uganda.

Mufuruki pia ana kampuni ya IIG Retail Limited inayouza na kusambaza nguo zenye nembo ya Levi’s.

Juhudi za Serikali ya sasa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ni miongoni mwa vitu ambavyo Mufuruki alivipigania hata akawa mwenyekiti wa kwanza wa shirika hilo wakati linaanzishwa kabla ya kusuasua na baadaye kufufuliwa na Rais John Magufuli.

Mufuruki ambaye amekuwa mwenyekiti wa mashirika mbalimbali, Agosti alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa Vodacom aliyoiongoza tangu Novemba 2017 na ameiacha ikiwa na mafanikio makubwa.

Miaka mitatu baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzishwa, Mufuruki aliteuliwa kuwa mjumbe wa kusikiliza mapendekezo ya kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo wafanyabiashara wanaokidhi vigezo wanaendelea kuilipa mpaka sasa.

Alivyopenda Afrika iendelee

Mufuruki aliwataka viongozi wa Afrika kuzitumia kwa manufaa rasilimali zilizomo barani humo na kubainisha namna alivyotaka kuziona nchi za Afrika zikipiga hatua kimaendeleo.

Mufuruki alishiriki makongamano ya maendeleo ya Taasisi ya Uongozi Institute na Agosti 29 ilipojadili umuhimu wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali wakiwamo marais wastaafu; Benjamin Mkapa (Tanzania), Olusegun Obasanjo (Nigeria), Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar huku Rais Magufuli akiwa mgeni rasmi, alibainisha dukuduku lake.

Bila kumung’unya maneno Mufuruki alisema aliwahi kutembelea makao ya Umoja wa Afrika (AU) nchini Ethiopia na kuelezwa kwamba viongozi wengi wa Afrika hawapendi kuhudhuria mikutano badala yake hutuma wawakilishi ingawa hupenda kuhudhuria inayofanyika Ulaya, Marekani, China au Japan.

Wakiwa hapo, alisema walielezwa kuna maazimio 1,400 yaliyopitishwa lakini miaka mingi imepita na hakuna nchi iliyoyatekeleza.

“Afrika ni kama msichana mrembo anayewaniwa na wanaume wengi kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa mataifa makubwa, ni lulu kwa kila taifa kubwa,” alisema.

Imeandikwa na Noor Shija, Julius Mnganga, Elias msuya na Asna Kaniki.