Idris Sultani amuomba msamaha Rais Magufuli

Thursday November 14 2019
idriss pic

Dar es Salaam. Msanii  wa vichekesho, Idris Sultan, amemuomba  msamaha Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kitendo chake cha kujifananisha naye na kuweka picha yake katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Idris ameomba msamaha leo Alhamisi Novemba 14, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari, akibainisha kuwa picha aliyoiweka haikuwa na maana mbaya kama ilivyotafsiriwa.

Msanii huyo anadaiwa kujifananisha na mtu mwingine na kuchapisha taarifa za uongo kwa kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.

Baada ya kufanya hivyo mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimtaka kuripoti kituo cha polisi jambo ambalo msanii huyo alilizingatia. Tayari amesharipoti polisi mara tatu. Jumatatu Novemba 18, 2019 anatakiwa kuripoti tena kituo cha polisi kati.

Katika mkutano wake wa leo,  Idris amesema yeye ni msanii ana njia nyingi za kufikisha ujumbe na alichokifanya ni ubunifu wake akilenga kumfikishia Magufuli salamu ya siku yake ya kuzaliwa.

Advertisement

Amesema kutokana na rais Magufuli kuwa na shughuli nyingi, alitumia picha aliyojifananisha na rais akiwa sehemu yenye utulivu ili aweze kusherehekea siku yake ya kuzaliwa bila kutingwa na majukumu mengine.

"Pamoja na nia yangu hiyo nzuri kwa bahati mbaya imetafsiriwa ndivyo sivyo na kama binadamu nimeona nimuombe Rais mwenyewe msamaha kwa picha ile kama ilimkwaza," amesema Idris.

Kuhusu kuhojiwa polisi, amesema jalada lake limepelekwa kwa mwendesha mashtaka wa Serikali (DPP)  kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya polisi kumaliza upelelezi wao.

Alipoulizwa kama haogopi kuweka picha ya rais mstaafu Benjamin Mkapa inayofanana na iliyosababisha akahojiwa polisi, amesema haoni kama ni tatizo.

Juzi Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa alizindua kitabu chake cha Maisha Yangu, Kusudi Langu chenye picha yake mbele. Sultan ameweka kitabu hicho katika mtandao wake wa Instagram na kubadili maneno pamoja na picha ya rais huyo mstaafu, kuweka ya kwake.

 

Sakata lake lilivyokuwa

Mkasa ulianza kama masihara kwa Idris kuweka katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia katika mtandao huo na kumtaka mchekeshaji huyo wa vituko vya ‘Sio Habari’ kujisalimisha polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” aliandika Makonda.

Baada ya mkuu huyo wa mkoa kueleza hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk  Hamisi Kigwangalla alishindwa kuvumilia badala yake akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi. Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”

Alipozungumza na Mwananchi baadaye kuhusu sakata hilo, Makonda alisema “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”

Kuhusu hatua ya Dk Kigwangalla kumwekea dhamana Idris iwapo atakamatwa, Makonda alisema “brother ile Twitt sikumuandikia mtu yeyote zaidi ya Idris, nenda kaisome vizuri.”

 

Advertisement