Imani za kishirikina zawatesa wanaougua fistula

Wednesday October 9 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Licha ya kuwa elimu kuhusu fistula imeendelea kutolewa kwenye jamii  na kuelezwa kuwa ugonjwa huo unatibika, bado kuna wanawake wanachelewa kupata matibabu kwa sababu ya Imani za kishirikina.

Hayo yameelezwa na Theodora Masako ambaye ni muuguzi anayehudumia wagonjwa hao katika hospitali ya CCBRT wakati Kwaya ya Gethmane ya Kanisa la SDA (Wasabato) Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Tanzania ilipowatembelea wagonjwa hao na kuwapatia msaada.

Masako amesema kuna changamoto kubwa ya wagonjwa kupata matibabu kwa wakati wakihofia gharama za matibabu huku wengine wakihusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina.

“Tumekuwa tukitoa elimu kuhusu ugonjwa huu ambao hauna uhusiano na ushirikina na wala matibabu yake hayana gharama yoyote ile na hapa kwetu tunatoa matibabu bila malipo. Nitumie fura hii kuishukuru kwaya hii ya Gethmane kwa kutambua umuhimu wa kutoa msaada wao kwa ajili ya wagonjwa hawa ambao tunawahudumia hapa hospitalini kwetu," amesema Masako.

Amesema wagonjwa wanapoona wanatembelewa wanafarijika na kuwapa moyo kuwa wapo watu ambao wanawathamini na kuwajali kwa sababu moja ya changamoto ya ugonjwa huo, ni wengi wao kutengwa na jamii na wakati mwingine hata na familia zao.

Mwalimu wa kwaya hiyo, Stella Malingoza amesema mwaka huu  kwaya hiyo inatimiza miaka 10 na wanajiandaa kuzindua DVD zao mbili Oktoba 13.

Advertisement

Hivyo, wameona ni vema kabla ya kufanyika kwa uzinduzi wakatoa msaada huo ambao ni sabuni, mafuta ya kupakaa, dawa za meno na miswaki.

"Tumekuwa na utamaduni wa muda mrefu wa kujitoa kwa misaada ya aina mbalimbali, tunaweza tusiwe tumetoa msaada mkubwa lakini kile ambacho tunakipata huwa tunakipeleka kwenye jamii ambayo ina uhitaji.

“Hivyo tumekuja CCBRT kwa ajili kuwaona mama zetu na dada zetu wenye kusumbuliwa na ugonjwa fistula na kadri tukavyopata tutarudi kwao na kwa wengine.Thamani vifaa hivi ni Sh2.4 milioni ,”

Kwa upande wake mchungaji wa kanisa hilo Masunya Athony  amesema  watu wanapokuwa wagonjwa si rahisi kwao  kupata neno la Mungu kwa usahihi, hivyo kwa kutambua hilo wameona kanisa lao lina wajibu wa kuwafikia wagonjwa na kuzungumza nao ikiwa pamoja na kushiriki nao maombi.


Advertisement