Jafo ataja vijiji, vitongoji upinzani uliposhinda

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo ameanisha baadhi ya maeneo ambayo vyama vya upinzani wameshinda licha ya viongozi wao wakuu kutangaza kujitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo ameanisha baadhi ya maeneo ambayo vyama vya upinzani wameshinda licha ya viongozi wao wakuu kutangaza kujitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Jafo alisema Chadema imeshinda vitongoji 27 katika mikoa mitano ikifuatiwa na CUF na ACT-Wazalendo iliyopata kitongoji kimoja katika mikoa hiyo.

Aliitaja mikoa na wilaya ambazo wapinzani wameshinda kuwa ni Kagera (Muleba DC),(Kibondo), Mara (Rorya), Rukwa (Sumbawanga DC), Nkasi DC na Sumbawanga Manispaa), Tabora (Igunga DC na Kaliua DC).

Kwa upande wa vijiji alisema vyama vya upinzani vilishinda nafasi katika mikoa mitatu ya Kigoma, Kagera, Rukwa katika halmashauri za Kibondo, Muleba na Nkasi zilizopo kwenye mikoa hiyo.

Chadema walipata kijiji cha Kitoko (Muleba) kilichopo kata ya Mubunda na vijiji vya Kasu na Ntamila vilivyoko wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

CUF ilifanikiwa kupata kijiji cha Kumkugwa kilichopo wilayani Kibondo, kwa mujibu wa Jafo.

Kwa upande wa vitongoji, Chadema ilishinda Kagera (9) vyote vikiwa katika wilaya ya Muleba, Kigoma (3) ambavyo vimepatikana katika wilaya ya Kibondo, Mara (2), Rukwa (8) sita vikiwa wilaya ya Nkasi na viwili Sumbawanga na Tabora (5).

Jafo alisema CUF walishinda Kagera (1), na Kigoma (1) na Tabora (1).

Kwa upande wa ACT-Wazalendo wamepata kiti kimoja tu mkoani Kigoma.