Jaji Warioba ataka utaratibu viongozi kuondoka madarakani uheshimiwe

Muktasari:

  • Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi na Watanzania kuendeleza utaratibu wa kiongozi kuondoka madarakani baada ya kumaliza muda wake ili kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.

Butiama. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi na Watanzania kuendeleza utaratibu wa kiongozi kuondoka madarakani baada ya kumaliza muda wake ili kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.

Jaji Warioba ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 14, 2019 katika mdahalo wa  ‘Nilivyomfahamu Nyerere’  uliofanyika  nyumbani kwa Mwalimu Nyerere Butiama mkoani Mara, ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo chake na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu waliowahi kufanya kazi naye.

Jaji huyo mstaafu ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia mjadala unaoendelea nchini wa  kuondoa ukomo wa uongozi, “ukiona kuna mabadiliko (ya katiba kuondoa ukomo) ujue kiongozi wa juu ndiye ana uchu wa madaraka kutaka kusalia madarakani.”

"Hoja ya kubadili katiba kuondoa ukomo haikuanza leo. Wakati ule mzee Mwinyi (Ali Hassan- Rais wa Awamu ya Pili), ikaja tena wakati wa Benjamini Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) na hata kipindi Jakaya Kikwete. Lakini wote walikataa na kuondoka madarakani muda wao ulipoisha kwa mujibu wa katiba.”

Ameongeza, “hata sasa wameanza kusemasema lakini bahati nzuri Rais John Magufuli ameshasema wazi kuwa hataki (kubadili katiba kuondoa ukomo wa uongozi). Nadhani tuendeleze utaratibu huu (kukabidhiana vijiti) kumuenzi  Mwalimu Nyerere,"