Jalada kesi ya Shamimu na mumewe bado linachapishwa

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili  mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida na mkewe, Shamim Mwasha umesema umejulishwa na polisi kuwa jalada la kesi hiyo bado linachapishwa.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili  mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida na mkewe, Shamim Mwasha umesema umejulishwa na polisi kuwa jalada la kesi hiyo bado linachapishwa.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai leo Ijumaa Agosti 30, 2019 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Simon amedai wamepewa taarifa na polisi  kuwa jalada la kesi hiyo linaendelea kuchapishwa na wanasubiri majibu ya kielelezo kutoka kwa mkemia mkuu wa Serikali ambacho ni dawa ya kulevya aina ya Heroin.

Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Shamimu ambaye ni mmiliki wa Blog 8020 Fashion na mumewe wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

Washitakiwa hao wakazi wa Mbezi Beach walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Mei 13, 2019 wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70

Inadaiwa Mei Mosi, 2019 wakiwa eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam walisafirisha dawa hizo.