Jalada la kesi anayetuhumiwa kumuua mkewe, kumchoma moto linachapwa

Monday November 18 2019

 

By Pamela Chilongola na Mainda Mhando, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara Hamis Said Luongo umedai jalada la kesi hiyo linaendelea kuchapwa na likikamilika litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DDP) ili taratibu za kisheria zifuatwe.

Luongo anakabiliwa na  kosa la kumuua na kumchoma moto kwa magunia mawili ya mkaa aliyekuwa mkewe Naomi Marijani.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai leo Jumatatu Novemba 18, 2019 kuwa alishaieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi umekamilika hivyo anaiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

"Kutokana na jalada la kesi hii kuendelea kuchapwa na baada ya kukamilika linatakiwa lipelekwe  kwa DDP ili taratibu zingine za kisheria zifuatwe," alidai Simon.

Naye Wakili wa utetezi, Mohammed Majaliwa  alidai hawana pingamizi na ombi hilo lililotolewa na upande wa jamhuri.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Salum Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Advertisement

Mshtakiwa huyo ameshtakiwa chini ya Kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Katika kosa hilo, mshitakiwa anadaiwa Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole Kigamboni Dar es Salaam alimuua mtu anayeitwa Naomi Marajani.

Inakumbukwa Hamis anadaiwa kumuua mke wake Naomi kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ambapo alichukua majivu ya marehemu na kwenda kuyafukia shambani kwake Mkuranga mkoani Pwani.

Advertisement