Jalada laendelea kuchapwa kesi ya anayedaiwa kumuua mkewe kwa kumchoma moto

Monday December 2 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa kuwa jalada la kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara, Hamisi Saidi (38), lipo katika hatua za mwisho kukamilisha kazi ya uchapwaji.

Hamisi Said anadaiwa kumuua Naomi Marijani ambaye ni mke wake na kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na baadaye kuchukua majivu yake na kwenda kuyafukia shambani.

Wakili wa Serikali, Tully Helela ameieleza Mahakama hiyo, leo Desemba 2, 2019, wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Helela amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally kuwa wanasubiri jalada hilo likamilike kuchapwa ili kesi hiyo iweze kuendelea kwa hatua nyingine.

“Upelelezi wa kesi hii umeshakamilika na kwa sasa tunasubiri jalada hili likamilike kuchapwa ili tuweze kuendelea na hatua nyingine kutokana na hali hii, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama uchapaji umekamilika,” alisema Helela.

Baada ya kuieleza Mahakama hivyo, Wakili wa utetezi, Mohamed Majaliwa alisema  hana pingamizi juu ya maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka.

Advertisement

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 16, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, Luwongo anakabiliwa na kesi ya mauaji namba 4/2019 iliyopo mahakamani hapo.

Anadaiwa kuwa Mei 15, 2019 katika eneo la GezaUlole, wilaya ya Kigambo, mshtakiwa alimuua mkewe aitwaye Naomi Marijani.

Advertisement