Jalada mashtaka ya Lissu mikononi mwa AG

Mgombea wa urais wa Chadema, Tundu Lissu

Muktasari:

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema jalada la mashtaka linalomhusu aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu na wenzake la kupanga kufanya maandamano bila kibali limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa hatua zaidi za kisheria.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Tundu Lissu kukamatwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana, jalada la mashtaka yake limetua mikononi mwa Mwanasheria mkuu wa Serikali.

Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema leo Jumanne Novemba 3, 2020 kuwa jalada hilo linalomhusu Lissu na wenzake wawili tayari limepelekwa kwa AG kwa hatua zaidi za kisheria.

Lissu alikamatwa jana jioni akiwa na wenzake wawili wakitokea ofisi za Umoja wa Ulaya zilizopo jijini Dar es Salaam na kuachiwa saa chache baadaye.

Kwa mujibu wa Mambosasa, Lissu anatuhumiwa kupanga na kufanya maandamano nchini bila kufuata utaratibu.