MAWAIDHA YA IJUMAA: Janga la corona kwa mtazamo wa dini ya Kiislamu

Tangu kudhihiri kwa janga la corona katika nchi mbalimbali duniani na hapa kwetu nchini, kumekuwa na maswali mengi yanayohitajia majibu hasa katika upande wa kiimani wa dini ya Kiislamu.

Ni vyema leo katika ukurasa huu wa mawaidha ya Kiislamu tukayapitia baadhi ya maswali na kuyapatia majibu japo kwa ufupi ili jamii isije ikakata tamaa na hatimaye kutumbukia katika janga kubwa zaidi la kiimani kuliko corona.

Swali la kwanza: Je, corona ni adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu au ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine? Jibu ni kwamba Corona ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine na pia ni adhabu kutoka kwa Mola wetu Muumba kwa waja wake waliopitiliza katika kutenda mambo maovu na machafu.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Hayatadhihiri Faahisha (madhambi ya zinaa na kulawitiana wanaume kwa wanaume na wanaume kuwalawiti wanawake) katika jamii, kisha wakayafanya hayo (madhambi) waziwazi ila itaenea kwao Twaauun (maradhi yanayoenea kwa mpigo) na magonjwa ambayo hayakuwepo katika zama za watu waliopita nyuma”.

Kutokana na jamii ilivyo sasa hapa nchini kwetu na huko nje kwa wenzetu, madhambi ya zinaa na kulawitiana sio tu kwamba yanafanywa bali yanatangazwa na yanahalalishwa kiasi cha kuwekewa sheria maalum kuhalalisha ndoa za jinsi moja, na jamii haikemei.

Kwa muktadha huo, corona ambayo kwa sasa ni janga kubwa duniani inaonekana waziwazi kuwa ni ugonjwa na adhabu kutoka kwa Mola wetu Muumba.

Kwa upande wa corona kuwa ni ugonjwa, suluhisho lake ni kujikinga kwa kuyashika na kufuata maelekezo yote yanayotolewa na mamlaka za Serikali kuhusu janga hili.

Ikiwa ni adhabu kutoka kwa Mola wetu Muumba, suluhisho ni kila mmoja wetu kufanya toba ya dhati yaani kutubia kwa Mola wetu Muumba kwa kuahidi kukoma (kuacha) madhambi na kuomba msamaha mara kwa mara na kamwe tusikate tamaa Mola wetu atatupokea, atatukubali na atatuondoshea janga hili na mengineyo.

Swali la pili: Kwa kuwa imethibiti kwamba maradhi haya yanaambukiza tena kwa njia nyingi, kwa nini kufunga nyumba za ibada hakukupewa nafasi hasa misikiti?

Jibu ni kwamba wanaoswali misikitini wanagawika katika makundi mawili: kundi la kwanza ni lile ambalo mazingira ya nyumba zao na maeneo yao ya kazi yanawaruhusu kuswali na kundi la pili ni lile ambalo mazingira ya nyumba zao na kazi zao hayawaruhusu kuswali peke yao.

Kulifungia misikiti kundi hili la pili maana yake ni kuwazuia kufanya ibada. Kwa mfano, watu wanaofanya kazi viwandani au katika karakana za magari au ‘wamachinga’ au wafanyabiashara masokoni au madereva wa daladala na kadhalika, endapo misikiti ikifungwa maana yake hawa wote hakuna kabisa kwao kuswali wakati Swala ni ibada ambayo haitakiwi kuachwa hata vitani.

Ni vyema Watanzania wanaopendekeza nyumba za ibada zifungwe wajibainishe kwani wao kabla ya janga la corona walikuwa wanaswali? Je, wanafahamu uzito wa ibada ya Swala?

Ieleweke kwamba misikiti ndipo mahala patukufu pa kumlilia Mwenyezi Mungu na yeye Mwenyezi Mungu yupo karibu sana na waja wake wanaposujudu. Hivyo sio sahihi katika wakati huu wa dhiki kuwaepusha Waumini na eneo zuri na tukufu la kufanyia maombi.

Pia, ni vyema wanaofikiria kufunga nyumba za ibada wakajiuliza: Je, masoko pia yafungwe? Je, viwanda vifungwe? Je, mabasi yazuiwe yasibebe abiria? Je, hospitali zifungwe? Je, tukifunga sehemu zote hizo watu wabakie nyumbani, hivi wamefanya maandalizi ya kutosha ya chakula na mahitaji mengine muhimu?

Swali la tatu: Je, corona ni maradhi ya kutengenezwa au ni mpango wa Mwenyezi Mungu? Jawabu ni kwamba jambo lolote lililopo na litakalokuwepo duniani liwe limetengenezwa au limezuka lenyewe, hilo limo katika mpango wa Mwenyezi Mungu (Qadar).

Katika Uislamu, nguzo za imani ni sita na mojawapo ni kuamini Qadar (mpango wa Mwenyezi Mungu), kheri zake na shari zake kwamba vyote vinatoka kwake. Mwenyezi Mungu anatuambia katika Quran Tukufu Sura ya 9 At-tawbah) Aya ya 51:

“Sema: Halitotupata ila lile alilotuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na kwa Mwenyezi Mungu tu wategemee Waumini”.

Imani thabiti ya kidini ni kuamini kwamba kila jambo limo ndani ya mpango wa Mwenyezi Mungu. Hivyo Waumini wanapaswa kuwa na subra wasifadhaike na wajenge imani thabiti kwamba alitakalo Mola ndilo litakalokuwa. Kwa kuhitimisha, mafunzo ya Dini ya Kiislamu yanatuelekeza kujikinga na kujitibu katika maradhi yoyote yale. Hivyo kuchukua tahadhari ni sehemu ya mafunzo ya dini, Ndio maana Muislamu akienda chooni huwa anajikinga, anaomba dua kwa kusema: “Ninajikinga kwa jina la Mwenyezi Mungu kutokana na shari za mashetani wanaume na mashetani wanawake”.

Kwa upande wa kujitibu (dawa), tumefundishwa na Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) pale aliposema: “Jifanyieni dawa enyi Waja wa Mwenyezi Mungu, hakika Mola hajaweka ugonjwa illa ameuwekea dawa”.

0754 299 749/ 0784 299 749