Jennifer Lopez, Shakira jukwaa moja Super Bowl 2020

Muktasari:

Watatumbuiza wakati wa mapumziko ya fainali ya Ligi ya Mpira wa Kikapu wa Kimarekani (NFL) inayokutanisha bingwa wa kanda mbili na itakayofanyika Miami.

 


Wanamuziki wawili wanawake, Jeniffer Lopez na Shakira watachangamsha jukwaa wakati wa mapumziko ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mpira wa Kikapu wa Kimarekani (NFL), maarufu kwa jina la Super Bowl itakayofanyika Miami Februari 2, 2020.

Super Bowl ni jukwaa kubwa la starehe duniani linalokutanisha pamoja michezo, burudani na biashara, likiingiza mabilioni ya fedha kwa waandaaji kutokana na matangazo yanayorushwa wakati wa mchezo huo, viingilio na fedha za haki za matangazo ya televisheni.

“Tangu nimuone Diana Ross akitokea angani kuingia uwanjani katika onyesho lake wakati wa mapumziko, nimekuwa nikiota kupata nafasi ya kutumbuiza Super Bowl,” alisema Lopez akikaririwa na gazeti la Los Angeles Times la Marekani.

“Na sasa imekuwa kitu maalumu na si tu kwa sababu ni mwaka wa 100 tangu NFL izaliwe, bali kwa sababu natumbuiza na mwenzangu kutoka Amerika Kusini. Ninasubiri kwa hamu kuonyesha kile wanawake wanachoweza kufanya kwenye jukwaa kubwa duniani.”

NFL, Pepsi na Roc Nation zilitangaza Septemba 26 kuwa nyota hao, ambao wamekuwa wakitoa nyimbo zao kwa lugha ya Kiingereza na Kilatini tangu miaka ya tisini, watatumbuiza katika mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Hard Rock katika jimbo la Florida.

Shakira pia ameonyesha kufurahishwa na mafasi hiyo.

"Nimepewa heshima kubwa kutumbuiza katika moja ya majukwaa makubwa duniani pamoja na Mlatini mwenzangu ili kuwawakilisha Walatini waishio Marekani na sehemu nyingine duniani — na kuongezea zaidi, siku hiyo ni siku yangu ya kuzaliwa!” alisema Shakira.