Jimbo Katoliki Moshi lapata askofu mpya

Monday December 2 2019

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Mhashamu Baba Askofu Ludovick Joseph Minde kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi.

Mpaka uteuzi huo unafanyika, Mhashamu Minde alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama tangu mwaka 2001 baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu, Yohani Paul wa II.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Desemba 2, 2019 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Charles Kitima imeeleza kuwa uteuzi huo umetangazwa leo na Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania.

Askofu Minde alipata shahada ya Uzamivu nchini Italia akiwa daktari katika Teolojia ya Maandiko Matakatifu.

Pia, baada ya kumaliza masomo hayo mwaka 1996, alirejea nchini akiwa Mhadhiri wa Teolojia ya Maandiko Matakatifu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwaga iliyoko Segerea Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 2001, alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Advertisement

Mteule huyo ambaye amezaliwa mwaka 1952 Kibosho, Moshi Mkoani Kilimanjaro alipata elimu ya msingi katika shule ya Mweka na baadaye Seminari ya Mtakatifu James Junior alikomaliza kidato cha sita.

Alipata Daraja ya Upadrei mwaka 1986 katika Shirika la Kazi la Roho Mtakatifu na kuwa mlezi wa vijana wanaotaka kujiunga na shirika.

Wasifu:

Askofu Ludovick Minde alizaliwa mwaka 1952. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadri  Juni 26, 1986.

Aprili 24, 2001, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, alimteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Agosti 5, 2001 na Kardinali Polycarp Pengo.

Desemba 2, 2019, Baba Mtakatifu Francisko amemteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi.

Advertisement